Habari MsetoSiasa

Mtajutia kukubali serikali ya mseto, Ruto aonya

July 22nd, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

NAIBU Rais William Ruto amepuuzilia mbali mapendekezo kuhusu serikali inayojumuisha washindani mbalimbali.

Akizungumza katika mahojiano na runinga ya K24, alisema kuwa iwapo hilo litafanyika, basi nchi itasalia kujuta.

Naibu huyo alionekana kutoa maoni hayo ambayo hayakulingana na matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta aliyotoa mwaka jana.

Rais alipendekeza kuwa ni vyema kwa taifa kuwekeza katika mfumo wa serikali ambapo watu hawang’ang’anii uongozi kiwango cha kuwatenganisha wananchi, akisema kuna nia ya kujumuisha jamii mbalimbali, ikiwa hilo litasuluhisha tofauti za kisiasa ambazo zimekuwa zikishuhudiwa kila baada ya uchaguzi.

Bw Ruto ametaja mapendekezo ya Rais kuwa ndoto, akisema hiyo ni njia ya kurejesha taifa kuwa la chama kimoja, hali aliyoitaja kuwa itafanya Kenya kuwa nchi ya kidikteta.

Alisisitiza kuwa sharti kuwe na mshindi na anayeshindwa katika uchaguzi ili uwe na maana, matamshi ambayo ni kinyume na alivyopendekeza Rais Kenyatta Desemba mwaka jana, alipokuwa eneo la Kisumu.

“Kenya ni taifa la kidemokrasia kwa kuwa na vyama vingi. Sidhani kuna utungaji wowote wa sheria ama ubadilishaji wa katiba ambao utabadilisha Kenya kutokuwa demokrasia ya vyama vingi,” Naibu Rais akasema.

“Baadhi ya mapendekezo ninayosikia watu wakitoa kuwa kama mbinu ya kuingiza kila mtu uongozini, washindani wawe wakishirikiana na serikali baada ya uchaguzi, nayapinga kwa kuwa huko ni kupendekeza tuwe nchi ya chama kimoja. Ikiwa hakutakuwa na mshindi katika uchaguzi, tunavyosema ni kuwa tunajaribu kuunda nchi ya chama kimoja. Tunajipeleka moja kwa moja kwa Udikteta,” Dkt Ruto akasema.

Aliendelea kukosoa mapendekezo hayo, badala yake akipendekeza kiongozi wa upinzani awe na afisi na awe akifadhiliwa na serikali, ili aendeleze kazi zake za kuikosoa serikali ipasavyo.

“Tusiwahi kufikiria kuwa na chama kimoja. Tunachofaa kufanya ni kufadhili upinzani ili ufanye kazi zake ipasavyo na kujukumisha serikali. Kile kimeyumbisha upinzani kwa sasa ni kuwa mshindani mkuu katika uchaguzi hana afisi mahususi, hapo ndipo tunafaa kurekebisha,” akasema.

Alisema hali hiyo ya kukosekana kwa afisi rasmi ya upinzani imeishia kumaliza nguvu zake, akiashiria unaelekea kumezwa na serikali.

“Kwa sasa sina uhakika ikiwa tuko na upinzani. Tunao waliokuwa viongozi wa upinzani kama Raila Odinga, ambao sasa wako mahali katikati; hawako upinzani tena,” Dkt Ruto akasema.

Kiongozi huyo alisema kwa sasa hakuna haja yoyote ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi, akisema hakuna kitu kikubwa kinachofaa kubadilishwa katika katiba, na kuwa machache yaliyopo yanaweza kufanyiwa hivyo bungeni.

“Tunachohitaji ni kuwa na upinzani thabiti nchini ili serikali ifanye kazi ipasavyo. Kulingana nami hapo ndipo tuko na pengo tu,” Naibu Rais akasema.