Habari Mseto

Mtalii ndani miaka 18 kwa kupapasa wasichana kutoka jamii maskini

July 19th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MTALII raia wa Uingereza aliyetumia pesa kuwadhulumu kimapenzi wasichana wenye umri mdogo akizuru Kenya amefungwa jela miaka 18.

Keith Morris, 72 mkazi wa Hull locksmith, Uingereza, alitumia nguvu zake kuwarai na kuwanajisi wasichana akitalii eneo la Pwani ya Kenya kati ya Januari 18, 2016 na Februari 2017.

Mahakama ilipata kwamba Morris alitenda kosa hilo japo alikuwa akiheshimiwa sana na wakazi masikini wa vijiji eneo la pwani alikopenda kutalii na hata alikuwa akiwapa misaada ya kifedha kusaidia wasichana kupata elimu na matibabu.

Akimhukumu kufungwa jela miaka 18 na nusu mnamo Jumatano, Jaji Mairs wa Mahakama ya  Leeds alimwambia: “ Ulikuwa ukisaidia wakazi wa kijiji hiki hasa watoto. Hakuna shaka kwamba ulitumia uwezo wako wa kifedha kuwafikia wasichana hao,”

“Uliwanyemelea wale waliokabiliwa na umasikini. Ushahidi ulionyesha kuwa wakazi wa kijiji hicho ni masikini sana na ulichagua waliolemewa na hali hiyo kuwadhulumu.”

Jaji alisema Morris alijifanya mfadhili wa wasichana hao ili kuficha vitendo vyake kwa kuonekana kuwa mtu wa heshima.

Alipatikana na hatia kufuatia kesi aliyoshtakiwa baada ya uchunguzi uliofanywa na Shirika la Taifa kuhusu Uhalifu na maafisa wa upelelezi wa Kenya.

Uchunguzi huo ulifanywa baada ya wanandoa kutoka Uingereza kumripoti kwa polisi walipogundua tabia yake ya kuwadhulumu watoto.

Morris alikanusha madai dhidi yake akisema alikuwa kama mzazi wa wasichana hao na kwamba walifurahia kuishi naye katika hoteli za kifahari alizokuwa akitembelea.

Hata hivyo, mahakama ilisema alikuwa akidandaganya na kumpata na hatia ya mashtaka manne ya ubakaji wa msichana waliokuwa na umri wa miaka 16.

Aidha, alipatikana na hatia ya kutaka kuzuia haki kutendeka kwa kutisha wasichana hao.

Mahakama ilipata kuwa alikuwa akiwapa zawadi wasichana hao na watu wa familia kabla ya kusaliti imani yao kwake kwa kuwatendea unyama watoto hao.

 Ilisema vitendo vyake vitawaathiri watoto hao katika maisha yao yote.