Mtambue ‘Kanini’ wa kipindi cha Maria

Mtambue ‘Kanini’ wa kipindi cha Maria

Na JOHN KIMWERE

SURA yake na hata jina, sio geni kwa wafuasi wa tasnia ya filamu hapa nchini. Ameodhoreshwa miongoni mwa wasanii wa kike wanaozidi kuvumisha jukwaa la burudani kupitia uigizaji na vichekesho. Amefanikiwa kuchota wafuasi wengi tu ambao wamefikia kumfuatilia anavyofanya uhondo wake katika sekta ya maigizo.

Alice Muthoni Mari ni kati ya wasanii wanaovumisha kipindi ambacho kimejizolea umaarufu sio haba cha Maria ambacho hupeperushwa kupitia runinga ya Citizen TV.

Kando na uigizaji mwana mama huyu ni mwanabiashara ambaye huuza bidhaa tofauti mtandaoni na ni mtunzi wa nyimbo za injili. Katika muziki mapema mwaka huu aliachia teke moja inayokwenda kwa jina ‘Hujaniacha.’

Dada huyu anafahamika kwa majina tofauti katika filamu mbali mbali ambazo amefanikiwa kushiriki tangia aanze kujituma katika masuala ya maigizo mwaka 2010. Mwigizaji huyu aliyezaliwa mwaka 1976 anafahamika kama Kanini (Maria) na Mama Joe (Baba yao).

”Binafsi nimeshiriki filamu nyingi za lugha ya Kikuyu ambazo hupeperushwa kupitia Inooro TV,” alisema na kuongeza kuwa amepania kuwa kielelezo kwa waigizaji chipukizi kwa kuwadhirihishia kuwa kuna njia licha ya pandashuka nyingi tu ambazo hupitia kwenye juhudi za kusaka ajira.

Mama huyu ambaye katika ndoa yake wamebarikiwa na watoto watatu, anasema tangia akiwa mtoto alitamani kuwa mhasibu alivutiwa na uigizaji baada ya kumtazama Miss Morgan alivyokuwa akishiriki katika kipindi cha Tahidi High.

Alice Muthoni Mari maarufu Kanini wa kipindi cha Maria.

Kando na kipindi cha Maria kinaozidi kuwapa uhondo mashabiki wa maigizo nchini, kanini anajivunia kushiriki filamu zingine ikiwamo ‘Fashion Show,’ ‘Maharajah,’ ‘Inspekta Mwala,’ (Citizen TV), ‘Baba yao,’ (KTN home),’ ‘Anda Cover,’ ‘Mafundi,’ (NTV), ‘Njoro wa uba,’ na ‘Varshita,’ zote (Maisha Magic) na ‘Centrosinema,’ (Inooro TV).

Kando na kampuni ya Jiffy Pictures ambayo ndio huzalisha kipindi cha Maria, kisura huyu pia anajivunia kufanya kazi na makundi kadhaa kama Rescue Media, Advanced Pictures, Moon Beam na Discovery kati ya mengine.

Mwigizaji huyu tayari ameanzisha brandi yake inayokwenda kwa jina Elijones Pictures ambapo anasema kuna projekti anazofanyia kazi. ”Nachukua nafasi hii nishukuru wafuasi wetu kwa jumla maana siku hizi hali imebadilika kiasi kinyume na ilivyokuwa miaka iliyopita,” akasema.

Anashauri wenzake wafahamu kuwa hakuna kizuri hupatikana rahisi lazima wajitume kuchapa shughuli bila kulegeza kamba. ” Sina shaka kuwashauri kuwa wasitegemee kudanganywa na maprodusa kuingia katika mitego yao kuwa na mahusiano ya kimapenzi nao wakihaidiwa kupata ajira.

Katika mpango mzima nawahimiza wanadada wasanii wenzangu wakome kuwapa nafasi wanaume kuwashusha hadhi kwa ahadi za kupata ajira. Kimsingi wanastahili kufahamu uigizaji ni talanta wala sio kazi ya ofisini.

Pia anatoa wito kwa serikali itambue nafasi ya sanaa ya uigizaji na kuanzisha mikakati itakaosaidia kuinua sekta hiyo ili kunufaisha wahusika. Kanini anasema anatambua uigizaji kama ajira maana inalipa wengi wanaume kwa wanawake. Katika mpango mzima anasema amekubana na changamoto kadhaa ikiwamo kutolipwa vizuri pia maprodusa kusepa bila kuwalipa chochote licha ya kufanya kazi.

You can share this post!

Fida-K yalalamikia ongezeko la mauaji ya wanawake Kenya

Tulianza vibaya lakini tuna matumaini tutamaliza vyema...