Michezo

Mtambue mfungaji mchanga zaidi katika historia ya Dortmund

September 15th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI Jude Bellingham alitangaza ubabe wake dimbani kwa kufunga bao katika mechi ya kwanza iliyoshuhudia waajiri wake Borussia Dortmund wakisajili ushindi mnono wa 5-0 dhidi ya MSV Duisburg katika raundi ya kwanza ya German Cup.

Bellingham, 17, alisajiliwa na Dortmund kutoka Birmingham City kwa kima cha Sh4.2 bilioni mnamo Julai 2020.

Mnamo Agosti 2019, kinda huyo alivunja rekodi ya mvamizi wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Trevor Francis kwa kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa katika kikosi cha kwanza cha Birmingham akiwa na umri wa miaka 16 na siku 38 pekee.

Jadon Sancho aliwafungulia Dortmund ukurasa wa mabao kupitia penalti ya dakika 15 kabla ya Bellingham kufanya mambo kuwa 2-0 katika dakika ya 30.

Kadi nyekundu ambayo Dominic Volkmer wa Duisburg alionyeshwa ililemaza kabisa uthabiti wa wenyeji wa Dortmund ambao walifungiwa mabao mengine na Erling Braut Haaland, Gio Reyna na Marco Reus katika dakika za 39, 50 na 58 mtawalia.

Licha ya Sancho kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kutua Man-United, Dortmund wamesisitiza kwamba Mwingereza huyo atasalia ugani Signal Iduna Park hadi kikosi kinachomhemea kiweke mezani kima cha Sh15 bilioni ndipo washawishike kumwachilia.

Mabao kutoka kwa Sancho na Bellingham yalimaanisha kwamba wanaweka historia ya katika kikosi cha Dortmund kuwa wanasoka wawili raia wa Uingereza kuwahi kupangwa katika kikosi cha kwanza na kila mmoja wao kufunga bao.

Goli la Bellingham lilimweka katika historia ya miaka 110 ya Dortmund kwa kuwa mwanasoka mchanga zaidi kuwahi kufungia bao miamba hao wa soka ya Ujerumani.

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO