Mtambue msanii chipukizi anayetunga nyimbo kwa lugha sita tofauti

Mtambue msanii chipukizi anayetunga nyimbo kwa lugha sita tofauti

Na WINNIE A ONYANDO

Msanii chipukizi wa mdundo wa Swahili RnB Andrew Kibera almaarufu Andy Saharan ana mengi yasiyo ya kawaida.

Andrew, 22 sasa, aliyevuma sana kupitia kibao chake cha ‘Never Let Go’ mwaka wa 2018 tayari ametunga nyimbo zaidi ya 30.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, kijana huyo alifichua kuwa ameweza kutunga na kuimba kwa lugha sita tofauti.

Katika mwaka wa 2018, kijana huyo alikuwa amemaliza masoma yake ya Kidato cha Nne na tayari alikuwa ametunga nyimbo 13.

Baada ya kukamilisha masomo yake ya sekondari, Andrew alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta (Bewa la Ruiru) anakosomea Sanaa ya Filamu na Uigizaji. Kijana huyo ni wanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho.

Masomo yake katika Sauti Academy (taasisi ya wanamuziki) yalikatizwa baada ya vyuo na matasisi kufungwa kutokana na ugonjwa wa corona.

Kijana huyo alipohojiwa mwaka wa 2018, alikuwa hajazamia uanamuziki jinsi alivyoimarisha na kukuza talanta yake katika muziki.

Muziki zake za hapo awali zilichukua mdundo wa Swahili RnB, Afro Soul, Afro Pop na Modern Rumba, hali ambayo hajabadilisha katika muziki zake za kisasa.

Anasema kuwa anapenda aina hizo za midundo kwa kuwa hutuliza na kuliwaza msikilizaji.

Andrew alikutana na wasanii ambao wamekuwa kielelezo katika maisha yake ya usanii. Msanii Joseph Ng’ang’a alimsaidia katika utoaji wa albamu yake ya kwanza ‘Never Let Go’.

Kukutana kwake na Lafrik Band pia imekuwa nyota la heri kwa mwanamuziki huyo chipukizi. Kikundi hicho cha Lafrik kimemwongoza na kumpa mawaidha jinsi ya kujiimarisha katika sekta ya muziki.

Andrew amepiga hatua nyingi sana katika ndoto yake ya kuwa mwanamuziki wa kutajika. Ameweza kurekodi nyimbo kumi na kutunga zaidi ya nyimbo thelathini tangua amalize shule ya sekondari mwaka wa 2018.

Andrew anatarajia kuzindua albamu sita mwezi wa Mei.

“Natarajia kuangusha albamu sita kali mwezi ujao, sasa hivi tunashughulikia video za hizo nyimbo,” alisema Andrew.

Majawapo wa wimbo anayotarajia kutoa mwezi ujao ni ‘SenaLwanyi’ ambayo inamaanisha ‘Toka Nje’. Ujumbe katika wimbo huo ni kuwahimiza waliojifungia ndani watoke nje wavute hewa tofauti na ya nyumba.

Nyimbo hizo ameweza kuzipakia katika mitandao ya kijamii kama vile YouTube, Audiomack, Soundcloud, Spotify na iTunes.

Japo Andrew anatoka katika jamii ya Waluo, yeye hupenda na kuenzi lugha zingine. Ameweza kutunga na kuimba nyimbo kwa lugha ya Kiluo, Kikuyu, Kimeru, Kiluhya, Kiswahili na Kiingereza.  Ameweza pia kujifunza Kifaransa.

Kando na kuimba, kijana huyo pia anapenda uigizaji jambo lililomfanya apate zawadi kemkem katika uigizaji akiwa katika shule ya Upili ya Kakamega Boys.

Kupitia uigizaji, kijana huyo pamoja na wenzake April 4, waliweza kuigiza mchezo wa ‘The Wizard Song’ ambayo waliiweka kwenye mtandao wa Facebook.

Kando na kuwa mwanamuziki, Andrew ni mwanabiashara. Anajikimu kupitia kuuza samaki. Anasema kuwa yeye husambaza samaki katika kaunti zingine jambo ambalo lilikatizwa baada ya Rais kufunga nchi kama njia ya kupunguza maenezi ya virusi vya corona.

Anaeleza kuwa mazingira yake ilichangia sana katika kusisimua ari yake ya kuimba. Wazazi wake ni wanakwaya kanisani. Yeye pamoja na wenzake wangeimba nyimbo za injili wakiwa wadogo ili kujifurahisha na kukuza sauti zao.

Andrew anasema kuwa wazazi wake wamekuwa wakimhimiza asisahau masomo yake na alikotoka hata baada ya kufaulu maishani. Wazazi wake pia wamemhimiza kutojilinganisha na mtu yeyote kwa kuwa kila mmoja ana lengo na njia tofauti maishani. Wazazi wake wamekuwa kwa upande wake wakati wote na kumpa mawaidha ya kila aina.

Andrew anawahimiza wafuasi wake wawe wenye subira na waendelee kusimama naye kwa hali na mali.

You can share this post!

Bei ya mafuta haitabadilika – Serikali

HAKUNA PUMZI