Mtambue msanii Geerah The Boy kutoka Pwani

Mtambue msanii Geerah The Boy kutoka Pwani

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

NI sababu mbili kuu ndizo zilizomfanya Gerald Mwendwa Nzomo ajiepushe kuimba nyimbo za karne ya kisasa na akaamu kujitosa kwenye kuimba nyimbo za kumsifu Bwana.

Nzomo almaarufu Geraah The Boy alianza kwa kuimba wimbo wa mapenzi mwanzoni mwa mwaka 2019 alipokutana na kipusa aliyeukosha moyo wake na kuamua kumuimbia wimbo wa ‘Sitakuacha’ akimaanisha kuwa atakuwa naye daima dawamu.

Baada ya wimbo huo, chipukizi huyo akaamua kutoa kibao cha ‘Mama’ ambacho mashairi yake yote ni yale ya kumsifia mamake aliyemlea kwa raha na shida hadi akafikia umri alionao wakati huu.

Sababu ya kwanza iliyomfanya awachane na kuimba nyimbo za karne ya sasa ni kuwa mpenzi aliyemtegemea kuufurahisha moyo wake, alimkosea na kuamua kuepukana naye.

Sababu nyingine iliyomfanya atoe uamuzi kamili wa kujiepusha kuimba nyimbo za mapenzi na kuimba nyimbo za Injili ni kutokana na kuzisikiliza nyimbo za mwimbaji mshuhuri wa nyimbo za dini anayeishi Nairobi, Guardian Angel.

“Kuepukana na mpenzi wangu aliyenikasirisha na kuzisikiliza nyimbo za Guardian Angel ndiko kulikonifanya niwe na ashki ya kuimba nyimbo za kumtukuza Mungu. Na ni uamuzi ambao nataka ubakie hadi pale nitakapoamua kuacha kuimba ama siku yangu ya mwisho kuwa duniani itakapofika,” akasema.

Geraah The Boy anasema kuwa moyo wake umetulia na anasikia utulivu tangu aanze kuimba nyimbo za Injili na ana matumaini makubwa ya kutaka kuendeleza kipaji cha uimbaji wake kufikia kile cha kimataifa.

“Nina waimbaji wengi ambao napenda kusikiliza nyimbo zao na hasa wale kina Yilma William, Bonny Muitege na Bahati Bukuiku wa Tanzania hali hapa nchini ni shabiki wa Guardian Angel na Kelvin Bahati kwa nyimbo zao za Inujili,” akasema msanii huyo.

Alipohojiwa ni kwa nini waimbaji wengi wakati huu wanakimbilia kujitosa kwenye nyimbo za Injili na sio kuimba nyimbo zinazovutia vijana wenzao, Geraah The Boy alijibu kuwa waimbaji wengi huwa wameona mwangaza na nyota zinawafikia wakiimba nyimbo za dini.

Mwimbaji huo alizindua wimbo wake wa kwanza wa Injili mnamo Februari, 2020 ambao ulikuwa ni ule wa ‘Nitabaki na wewe Mungu’ ambao uliitikiwa vizuri na ambao ndio ulimpa moyo wa kuzidi kutoa nyimbo zake nyingine tatu.

Nyimbo yake ya pili ilikuwa ni ile ya ‘Jipe moyo’ ambayo pia aliitoa mwaka jana. Mwaka huu, Geraah The Boy tayari amefanikiwa kutoa nyimbo mbili za ‘Asante Ngai’ aliyoimba kwa lugha ya Kikamba na nyingine ni ‘Niongoze’.

Msanii huyo anasema alikuwa na hamu kubwa ya kutumia mitindo ambayo inawavutia vijana ilia pate kuwaondoa kwenye maasia na wafuate mwendo anaopenda Mungu, lakini alifikiria kuwa akifanya hivyo, huenda akavutiwa kurudi alikotoka kwenye nyimbo za karne ya sasa.

Alitoa mfano wa baadhi ya wasanii ambao hakupenda kuwataja waliokuwa waimbaji wa nyimbo za dini lakini kutokana na mitindo waliyotumia, wakavutiwa na kubadili nyendo zao na kurudi kuimba nyimbo za mapenzi.

Geraah The Boy ana hamu kubwa ya kufanya kolabu na msanii mkubwa kwani anaamini akipata fursa hiyo, ataweza kutambulika haraka na kuwa maarufu. Lakini mbali na hivyo, ana mipango kabambe ya kutembelea sehemu nyingine za nchi kujumuika na waimbaji wenzake wa Injili kwenye tafrija mbalimbali.

Pia ana mpango baada ya nchi kufunguka kutokana na janga la corona kutembelea nchi jirani ya Tanzania kujaribu kujadiliana na wasanii maarufu wa Injili uwezekanao wa kuimba pamoja nao.

You can share this post!

Yanga SC yakaribia kumsajili raia wa Serbia

KIKOLEZO: Youtubers kimeumana