Mtambue mtangazaji wa soka chipukizi ‘Arocho’

Mtambue mtangazaji wa soka chipukizi ‘Arocho’

Na PATRICK KILAVUKA

Uwezo wa kutenda mambo unatokana na ufahamu au kujijua fika katika mintarafu ambayo uwezo wako upo! Hata hivyo, kuiga au kujifunza ni njia nyingine ya kujigundua zaidi katika taaluma au talanta.

Kwa hayo, mtangazaji chipukizi George Ekombe Odero “Arocho” alikuwa na uchu wa kupeperusha matangazo ya boli kama angali kinda. Lakini alipata ari ya kuamsha kipawa chake baada ya kupata chocheo na mshawisho kutoka kwa mtangazaji wa kabumbu Fred Orocho wa kituo kimoja cha redio nchini.Vile vile anaamini kwamba fuata nyuki kule asali. Aghalabu, amekuwa na uraibu wa kumuiga kukiwapo mechi za mtaani.

Odero anasema mikogo na uchongezi wa maneno ya mnato kwa mashikio ya mskilizaji wa mtangazaji huyo, yalimpelekea kutia bidii kujikuza kutangaza mithili ya chiriku huyo ambaye huchota hisia za wasikilizaji wengi viwanjani na kwenye radio kwa kuacha wengi wakivunja mbavu huku ajibatizia unabii wa mechi pasi na kusema haongezea chumvi wala mdarasani katika utabiri wake akiona magoli yakinukia au timu ikibwaga au kuibuka mshindi!

“Kauli zake Arocho, zilinipelekea kushika rada ya kuvuta hadhira uwanja nilipokuwa ninapeperusha matangazo ya mechi za mtaani, Kangemi hususa viputeni, “asema. Odero anayeamini kwamba atakuwa zalio ya kasuku mtangazaji aliyemtaja.

Mtangazaji chipukizi George Ekombe Odero (kulia, aliyevalia fulana nyekundu) akitangaza dimba la nusu fainali ya Tim Wanyonyi Super Cup- Leads United dhidi ya WYSA United uwanjani, City Park ..Picha/ Patrick Kilavuka

 

Alizaliwa Charinze, Mwanza, nchini Tanzania na kusomea Shule ya Msingi ya Siginda, kabla kuguria nchini na kujiunga na Shule ya Msingi ya Farasi Lane, Lower Kabete kisha Sekondari ya Mabole , kaunti ndogo ya Butere.

Alifufua matumaini yakuwa mtangazaji mwaka wa 2014 baada ya kutekwa kihisia na utangazaji wa mtangazaji huyo anayemhusudu. Anadokeza wakati huo alikuwa anapeperusha mechi kati ya Manchester City dhidi ya Lecieter United katika Ligi ya Uropa (EPL).

“Nilikuwa ninamfuata kenyekenye akitangaza. Nilijiundia kipaza sauti changu cha kutangazia. Baada ya mechi hii, niliwaza na nikajiamini kwamba safari ya kila kitu huanza na hatua moja. Nilianza kuenda viwanjani mtaani kujinoa pasi na kuwa na kushauku katika kutimiza ndoto yangu, ” aeleza Ekombe ” “Orocho” ambaye sasa kipawa chake kimepata mwanga kwani sasa ana uwezo wa kupeperusha matangazo ya mechi za mitaani kama mtangazaji anayeibukia.

Mwaka 2018, alipata fursa ya kutangaza fainali ya dimba Tim Wanyonyi Super Cup chini ya udhamini wa mbunge wa eneo la Westlands ambapo Leads United ilikuwa inagaragazana na Red Carpet uwanja chuo kikuu cha Kiufundi cha Kabete. Mirindimo ya pongezi alizopewa, anasema zilimtia motisha zaidi kuangazia utangazaji wake.

Angependa sana kumshukuru Tim Sande ambaye tangu mwaka 2019 baada ya kutambua uwezo na utajiri wa talanta yake, alianza kumpa fursa ya kupeperusha matangazo ya mechi za dimba la Tim Wanyonyi Super Cup huku akaanza kupata pato kama njia ya kuinua kipawa chake cha mtangazaji chipukizi.

Mwaka jana alipata fursa nyingine ya kupepperusha matangazo ya michuano ya robo- fainali hadi fainali na kudhihirishwa kwa jitihadi haiondoi kudura.

Aliweka hewani mechi za nusu fainali kati ya Leads United na WYS A United ambapo Leads iliibinya WYSA 3-0 kisha ule mgaragazano baina ya Leverkusen na White Eagles ambapo Leverkusen walibuka washindi matuta 4-1 baada ya sare ya 1-1 muda wa kawaida.

Hatimaye, alitangaza mechi za fainali ambazo ziliandaliwa uga wa CAVS, Kabete ambapo Madume wa Leads United walikwangura Leverkusen Penalti 4-2 baada ya kuagana sare ya 1-1 na akina dada wa Kangemi Ladies walisazwa na Kibagare Girls 2-1.

Dimba la fainali ya Tim Wanyonyi Super Cup kati ya Kibagare Girls – jezi ya kijani kibichi na Kangemi Ladies -jezi ya bluu uwanjani, CAVS, Kabete, ambapo George Ekombe Odero alikuwa akitangaza. Picha/ Patrick Kilavuka

Ekombe ambaye pia aliyekuwa winga wa Kibagare Slum anasema angependa sana kuwa mtangazaji mtajika siku za usoni hususa siku moja atangaze jukwaa moja na mtangazaji anayemhusudu Orocho na mwenzake Diblo mwana wa Kaberia.

Angependa pia kuwashukuru wahimizaji wake- timu meneja wa timu ya Kibagare Girls Itotia Karanja na kocha Harun ambao walishauri kutochukulia kipaji alicho kwa mzaha bali aweke bidii ya mchwa na ataona matunda ya jasho. Na kweli ana ushuhuda kwa hayo kwani, sasa ana uwezo na ujasiri wa kupeperusha michuano mitaani na kiu ya kutangaza hata kwenye radio. Pia, angependa kuwashukuru mashabiki wanao mtia moyo kuzidisha matumaini na kujifua zaidi akilenga hatima yake.

Isitoshe, angependa kusema kwamba ni furaha yake kutangaza mechi kwo kwote kule almradi apate posho lake la kila siku kwani kazi ni kazi!

Ujumbe wake ni kwamba vijana wanafaa kujifungua na kutumia taaluma zao kwa busara kupata riziki na wasiwe na kinyongo wanapoona wengine wakiinuka. Isitoshe, wajifunze kwa watangulizi wao.

George huachi wachezaji na mashabiki kukauka tu mbali yeye pia huwauzia Ici krimu kukata kiu wakati wa mchuano kama hasiki kipaza sauti kama njia mbadala ya kujikimu. Anasema kila hupata kwenye talanta yake ya utangazaji huinua kazi yake.

You can share this post!

Man-City watwanga Wolves na kufungua pengo la alama 15...

Pigo mkali wa Safari Rally akifariki