Habari

Mtangazaji nguli Mohammed Juma Njuguna amefariki

June 8th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA na PSCU

MTANGAZAJI maarufu wa redio Mohammed Juma Njuguna ameaga dunia Jumamosi baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Bw Njuguna aliyetambuliwa kwa weledi wake wa kutangaza mechi za soka alifariki akitibiwa katika hospitali moja jijini Nairobi.

Hadi kifo chake, alikuwa mtangazaji katika kituo cha Redio Citizen alichojiunga nacho mwaka 1999 kutoka Shirika la habari la Kenya (KBC).

Rais Uhuru Kenyatta ametuma salamu za pole kwa familia, jamaa, ndugu na marafiki wa Njuguna.

Kiongozi wa nchi amemtaja mwandishi huyo wa redio wa hadhi ya juu kuwa mtangazaji aliyebobea na mwasisi aliyetumia wajibu wake katika vyombo vya habari kuelimisha na kuwatumbuiza Wakenya hususan kupitia matangazo yake bora ya mpira.

“Tunasikitika kufutia kicho chake. Mohammed alikuwa mwandishi shupavu wa habari. Alikuwa mtu mzuri na kielelezo katika sekta ya uandishi wa habari na mshauri mkuu kwa waandishi wa habari chipukizi,” amesema Rais Kenyatta.

Rais amesema katika wakati huu wa majonzi, mawazo na maombi ya Wakenya yameelekezwa kwa familia, jamaa na marafiki wa Mohammed.

Akiwa KBC alijijengea jina kama mtangazaji shupavu wa michezo na hasa mechi za soka.

Mohammed Njuguna alikuwa mtangazaji wa kwanza kutangaza mechi za Ligi Kuu ya soka nchini Uingereza nchini Kenya.

Alikuwa ametangaza mechi za soka kwa zaidi ya miaka 40.

Mnamo mwaka 2010 alikabidhiwa tuzo ya Head of State Commendation na Rais mstaafu Mwai Kibaki kwa kutambua kazi yake katika uanahabari.

Mohammed alikuwa daima mchangamfu; hulka ambayo ilimfanya kupata marafiki wengi mashuhuri wakiwemo marais Daniel arap Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Aliwahi kufanya kazi katika shirika la habari la Uingereza.