Makala

Mtangazaji wa redio apanga kuoa ‘malaika’ pacha wasiotaka kutenganishwa

Na LABAAN SHABAAN September 4th, 2024 3 min read

MTANGAZAJI wa redio ya kijamii Wambaz Oleman Learat, mwenye umri wa miaka 26, anataka kuasi ukapera.

Licha ya maswali yetu kumwandama kutaka kujua kwa nini anakusudia kuwaoa wanawake wawili katika harusi moja, jibu lake limekuwa lile lile; kwake ni sawa na kumuoa mke mmoja.

Pacha, Anne Samken na Emily Salaon, wameamua hawawezi kutenganishwa, kwa hivyo, afadhali waolewe na mume mmoja.

“Nimepasua mbarika kuhusu habari hii kwa familia yangu ambayo haijakataa lakini wanauliza maswali mengi,” Oleman anaambia Taifa Leo.

“Kwamba hawajapinga, hiyo naichukua kama ‘ndiyo’ huku nikiwaambia namuoa ‘msichana mmoja’ tu kwani wanafanana kwa kila kitu.”

Japo Oleman anasema atawajengea kila mmoja nyumba yake katika boma moja, pacha wanadokeza itakuwa vigumu wao kukaa kando na barafu yao ya moyo.

Wambaz Oleman. PICHA | LABAAN SHABAAN

‘Utengano ni udhaifu’
“Sisi hatujawahi kutenganishwa tangu tukiwa shule ya chekechea,” anaeleza Salaon.

“Walimu walitutenganisha kwa mwaka mmoja tukiwa shule ya upili tukaishi kwa huzuni na upweke.”
Salaon anaeleza kuwa tukio lilifanyika mwaka wa 2021 walipokuwa shule ya upili.

Walimu waliomba wazazi wawatenganishe kwa sababu walikuwa wanashinda pamoja bila kuzingatia shughuli za masomo.

Wakati huu, walikuwa wanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Gatero.
Ili kuhakikisha wanafanya vizuri, wazazi waliwahamisha ambapo Anne alipelekwa shule ya Inooro Girls naye Emily akasomea Loise Nanyuki Girls kwa mwaka mmoja.

“Japo matokeo yetu yaliimarika, tulipata msongo wa mawazo sana tukifikiriana,” alikumbuka Emily akishikilia haiwezekani kamwe wao kukaa mbali mbali.

“Sisi tutalala katika kitanda kimoja na mume wetu akilala katikati yetu,” aliongeza Anne.

Ninaweza kuwatofautisha
Warembo hawa wanafanana sana na haikuwa rahisi kwa Oleman kuwatambua wakati walianza uhusiano mwaka wa 2023.

“Emily ana kicheko cha kuambukiza huku Anne akizungumza kwa ulaini wa kuvutia na kutuliza,” alikiri Oleman.
Tulipowauliza vidosho hawa kinachowatofautisha walikuwa na maoni yao mahususi tofauti na mchumba wao.
“Emily ni mpole anayependa kusikiliza sana zaidi ya kuongea huku mimi nikiwa mchangamfu,” alisema Anne.

Walikutana 2023

Kulingana na Oleman ambaye ni mwanahabari wa kituo cha Sidai FM, walikutana mara ya kwanza katika hafla za burudani kisha akavutiwa nao.

“Niliona wanafanana kwa kila kitu. Ukiuliza swali, wanajibu pamoja kwa maneno sawa!” alimaka.
“Hapo nikaanza kuwachumbia na wakanipenda.”

Sasa wamejuana kwa karibu miaka miwili. Oleman anaarifu kuwa hawezi kuongea na mmoja akamtenga mwenzake.

Imemlazimu kufungua kundi la mtandao wa WhatsApp ili wabonge pamoja kila wakati.

“Hata nikipiga simu, lazima niwajumuishe wote wawili,” alieleza akisisitiza kuwa ilibidi afanye utafiti wa kupenda pacha bila mapendeleo.

Harusi ya kitamaduni
Oleman anafichua kuwa posa na harusi zitafuata desturi ya jamii ya Maa na sasa yuko mbioni kutafuta mpambe atakayemsaidia katika mchakato huu.

“Mtihani wangu mkubwa ni kumchagua mpambe ambaye anaelewa maisha ambayo nimechagua na jinsi atanitunza na kuwatunza,” anatikisa kichwa.

Bwana harusi huyu mtarajiwa anasema, kulingana na utamaduni, msaidizi wa bwana harusi atakuwa na baraka za wazee za kumtunga mimba mke wake endapo hana uwezo wa kuzaa.

Kitamaduni, hali hii pia inawezekana kama mume amefariki na itahitaji mke awe na mume.

“Badala ya mpambe kurithi mke, basi hubidi wazee wa jamii ya Samburu wamchague jamaa wa karibu,” anaeleza huku akikiri kuwa katika karne ya sasa desturi hii inapigwa teke.

Mahari
Katika jamii ya Maa, Oleman anahitajika kutoa mahari ya ng’ombe saba wa kike na ngamia wawili.

“Sitaki kuchangiwa na mtu kuwaoa hawa malaika. Kama jamaa zao watataka pesa nitawauza mifugo wangu,” anafichua. “Kwa thamani ya sasa, ngamia mmoja ni sawa na Sh120,000 huku ng’ombe akiuzwa kwa angalau Sh53,000.”

Anne na Emily wameeleza kuwa familia yake sasa ina habari kuwa wanatarajia mwanaume afike kwao kwa utambulisho Desemba 2024.

‘Maharusi’ hawa wametokea eneo la Rumuruti, Kaunti ya Laikipia na walisoma katika Shule ya Msingi ya Rumuruti DEB.

Kwa sasa wao ni wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo cha uhasibu cha Kenya College of Accountancy.
Emily anasomea masuala ya Benki na Fedha huku Anne akiwa mwanachuo wa uhasibu maarufu CPA.

Umri mdogo

Anne anaarifu kuwa katika umri wa miaka 20 wamekomaa kuolewa wakirejelea kuwa hata wasichana wadogo zaidi yao wa jamii ya Maa huozwa.

“Sisi si wachanga. Tayari tuna vitambulisho na sisi ni watu wazima kwa hivyo wazazi wetu hawana shida na sisi,” alieleza Anne tulipomrushia swali la udogo wao.