Habari Mseto

Mtangazaji Weldon Kirui asikitika redio zimesheheni matapiko machafu  

April 15th, 2024 3 min read

NA PETER CHANGTOEK

WELDON Oriöp Kirui alijulikana mno kwa vipindi kadhaa alivyokuwa akiandaa alipokuwa KBC Redio Taifa.

Kwa sasa, ni mtangazaji katika redio ya Kitwek Fm, inayomilikiwa na Shirika la Utangazaji la Serikali – KBC.

“Nilizaliwa 1972 katika eneo la Langam, Nakuru, nikiwa kitinda mimba. Nilianza masomo yangu katika Shule ya Msingi ya Kiplokyi, kisha nikajiunga na Shule ya Sekondari ya Cheborge, Kaunti ya Kericho kutoka 1987 hadi 1990, nilipofanya mtihani wa KCSE,” aeleza Kirui.

“Kazi hii ya utangazaji nilianza nikiwa katika Shule ya Upili ya Cheborge, nikiwa Kidato cha Pili, Februari 1988. Nakumbuka vizuri sana kwa sababu niliandika habari wakati wa tamasha shuleni na kusomea wanafunzi wenzangu. Habari nilizozitunga zilihusu matukio mbalimbali shuleni kama wanafunzi kung’ang’ania vyakula, chai, porojo za shuleni, vijana waliokuwa wakiwahangaisha wengine, matukio kutoka karibu na Cheborge, kama vile kukamatwa kwa walevi, na kadhalika. Habari nilizitunga zilivutia wanafunzi na walimu kiasi kwamba nikaitwa mtangazaji. Niliendelea na utunzi na usomaji wa habari hadi nikamaliza masomo yangu ya shule ya upili, na ari ya kujibwaga katika uandishi wa habari ikawaka ndani yangu,” asimulia mtangazaji huyo.

Baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya upili, aliendelea kuandika barua za maoni kwa magazeti mathalani Taifa LeoDaily NationThe StandardKenya TimesThe Weekend Mail na Die Welt.

Baadaye akajiunga na chuo cha KIMC alikosomea taaluma ya utangazaji, utayarishaji wa vipindi na uandishi wa habari.

“Nikiwa KIMC nilipata fursa nzuri ya kuandika habari nyingi mno kwa magazeti. Pia, nilijifunza lugha ya Kijerumani kwa mara ya kwanza katika taasisi moja jijini Nairobi,” afichua.

Kirui alijiunga na KBC Februari 1997 na kufanya kazi katika idara mbalimali, ikiwa ni pamoja na kusoma salamu, kutayarisha vipindi kama ‘Je Wajua?’, ‘Darubini’ na ‘Mali Shambani’, miongoni mwa vingine vingi.

Kabla hajajiunga na KIMC, aliwahi kudumu katika Kenya News Agency (KNA) 1994 na ECK (kwa sasa IEBC) 1992.

“Nimebahatika kuzuru nchi ya Ujerumani kwa masomo ya ziada ambapo nilipewa cheti kwa jina ‘Fortgeschritten Diploma in Rundfunk, Presse und Radio Produktion.’ Nikiwa Ujerumani 2005, nilitayarisha vipindi vilivyosikika katika Sauti ya Ujerumani na Radio Deutsche Welle, idhaa ya Kimombo,” afichua Kirui.

“Kama kuna kipindi ambacho watu huuliza hadi wa leo ni kile cha Historia na Maendeleo nilichoanza kutayarisha 1999 hadi 2007. Hiki ni kipindi cha matukio ya kihistoria ya Kenya na ulimwengu kwa jumla kama ilivyosimuliwa na Mwanahistoria Peter Chemaswet na Dkt Kipkoeech araap Sambu, ambaye kwa sasa ni msimamizi mkuu wa redio ya Kass Fm International, Washington Amerika. Hiki ni kipindi ambacho watu walikuwa wakikipenda sana na hata Rais Mstaafu Hayati Daniel arap Moi alikuwa shabiki mkuu. Kipindi hiki kiligusia historia ya jamii ya Kenya, historia ya mashujaa kama Koitalel arap Samoei, Ole Nana, Waiyaki wa Hinga, Lwanda Magere, Mugo wa Kibiru, Wangu wa Makeri na mashujaa wengine.”

“Pia, tulihadithia kwa kirefu historia ya Wayahudi, mapenzi kati ya Rais Bill Clinton na Monica Lewinski, na vita vilivyokuwa kati ya Iraq na Muungano wa Mataifa. Hata hivyo, kipindi hiki kilichukua mkondo mpya wakati Dkt Sambu aliponisihi tusimulie historia ya kale ya Misri ya Egyptology, kwa Kimombo.

Dkt Sambu alisimulia jinsi Waafrika, hasa jamii ya Kalenjin, walivyokuwa wakitawala. Si tu Misri, bali pia Ulaya, Indo-China, Amerika, Australia, Japan, eneo la South East Asia, na hata Mesopotamia. Kipindi hiki kilikuwa na mashabiki wengi mno, kiasi kwamba 2002 tulipata barua kadhaa za pongezi kutoka balozi za Congo, Belgium na sehemu nyingi za dunia,” asema Kirui.

“Nilivutiwa na watangazaji kama Francis Bale (Radio Uganda), Omir Herr, Ahmed Mohammed (Sauti ya Ujerumani), James Njuguna, Said Ali Matano, Catherine Kasavuli, Hilda Odera, Mambo Mbotela, Martin Mule na wengine.”

“Kunazo ndaro ambazo ziko katika utangazaji. Uandishi wa habari huzingatia mambo fulani na huandikwa kwa mtindo fulani. Mwaka 1999, nilimwaalika kijana aliyekuwa na kipawa cha kutangaza. Kijana huyo, Naphtali Ndege, ambaye kwa sasa ni mtangazaji, aliiga sauti ya Mambo Mbotela akiwa katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta. Alijifanya kumwalika rais baada ya ziara ya ng’ambo. Mambo yalienda mrama kwa sababu sauti aliyoitoa ilikuwa ya Mambo Mbotela, na watu wengi walidhani rais kweli alikuwa JKIA, jambo lililozua utata serikalini. Wakubwa wengi walikimbia kwenye uwanja huo, wakidhani kweli rais alikuwa akitoka ziara ya ng’ambo. Nusra nimalizwe, licha kwamba ilikuwa ni kijana aliyekuwa na kipawa cha utangazaji. Siku hizi, watu wa kuiga sauti ya rais ni wengi, lakini wakati fulani ilikuwa ni kosa,” asimulia.

Je, wajua siri ya kubobea na kufanikiwa katika tasnia ya utangazaji na uandishi?

Kirui anashauri kuwa, mwandishi wa habari na mtangazaji sharti asome vitabu vingi na magazeti mengi ili aelewe yanayoendelea ulimwenguni.

“Nimekuwa nikisoma vitabu vingi mno ili kuongeza maarifa ya kutumiwa kwa redio. Hupenda kusoma sana hadi saa sita za usiku. Nimesoma Kitabu ‘Egypt: The Light of the World’ kilichoandikwa na Mwanaegyptolojia Gerald Massey, na kingine, ‘The Sirius Mystery’ kilichoandikwa na Robert K.G. Temple. Utangazaji pia unahitaji mtu ambaye hupenda kutembea na kuzuru nchi na hata ng’ambo.”

Anasema kuwa, siku hizi utangazaji umeborongwa mno, si kama zamani.

“Utangazaji kwa sasa haupo tena. Kila mtu ni mtangazaji, hata wanasarakasi ni watangazaji. Wafanyibiasha na wengine ni watangazaji. Ukifungua redio hutaamini unayosikia hewani. Hawazingatii maadili ya utangazaji, bali mada yao tu ni mambo kama mapenzi, kujamiiana, masuala ya familia na uchafu mwingi unaotapikwa redioni. KBC ni kituo cha kipekee ambacho watangazaji huchungwa sana na husikilizwa kwa makini na wakubwa na wasimamizi,” asema mtangazaji huyo.
Kirui awashauri wale wanaonuia kujiunga na tasnia ya utangazaji na uanahabari wasife moyo, na wasome kwa bidii.