Habari

Mtanzania anaswa JKIA akiwa na dhahabu ya Sh100 milioni

February 21st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

SHIRIKA la Kukusanya Ushuru nchini (KRA) Jumatano limenasa dhahabu ya thamani ya Sh100 milioni katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA), jijini Nairobi.

Dhahabu hiyo ilisemekana kubebwa na raia mmoja wa Tanzania na ilipatikana na maafisa wa forodhani kwa ushirikiano na maafisa wa usalama katika uwanja huo.

Dhahabu hiyo ya gramu 32,255.50 ilipatikana pamoja na hati ya malipo ya Sh100 milioni.

Mshukiwa huyo alikamatwa baada ya maafisa wa polisi kudokezewa na umma kulingana na taarifa ya KRA Jumatano.

Kulingana na shirika hilo, kusafirishwa kwa dhahabu hiyo kulikuwa kinyume cha sheria ya kusimamia forodha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Dhahabu hiyo imezuiliwa na KRA, huku uchunguzi zaidi kuhusiana na suala hilo ukianzishwa.