Kimataifa

Mteja amuua weita kwa kuchelewesha mlo

August 18th, 2019 1 min read

Na AFP

WEITA wa hoteli moja jijini Paris aliaga dunia baada ya kupigwa risasi na mteja ambaye alilalamikia kutohudumiwa haraka.

Polisi mjini humo wameanzisha uchunguzi kuhusu kisa hicho huku mteja huyo akitoroka baada ya mauaji hayo katika hoteli kwa jina Noisy-le-Grand.

Juhudi za kumwokoa mhudumu huyo mwenye umri wa miaka 28 aliyepigwa risasi kwenye mabega ziligonga mwamba kwa kuwa aliaga dunia hotelini humo kabla ya kufikishwa hospitalini.

Wahudumu wenzake walieleza kwamba mteja huyo alikosa subira baada ya chakula chake kuchukua muda mrefu kutayarishwa ndipo akachomoa bastola na kumpiga mwendazake risasi.

Tukio hilo liliwashangaza wahudumu na wauzaji kwenye maduka ya karibu, wengi wakihofia usalama wao wakiwa kazini.

“Ni tukio la kusikitisha. Hii hoteli huwa ni tulivu na ilifunguliwa miezi michache tu iliyopita,” akasema mwanamke moja.

Baadhi ya wenyeji wa mji wa Paris nao walidai kwamba visa vya uhalifu, ulanguzi wa dawa za kulevya na ulevi vimeongezeka sana mjini humo na kuhatarisha hali yao ya usalama.