Michezo

MTG waridhika na pointi nne baada ya mechi mbili

May 7th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanawake ya Moving The Goalposts (MTG) iliandikisha ufanisi wa pointi nne kutoka mechi mbili za Kundi A Ligi ya Taifa Daraja ya Kwanza msimu huu.

Warembo hao wa MTG waliandikisha mafanikio hayo baada ya kunyamazisha kikosi cha Soccer Sisters kwa mabao 2-1 kisha kutoka nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya Limuru Starlets.

Lorna Nyarinda alitangulia kuiweka Sunderland Samba kifua mbele kabla ya Mukuru Talent Academy kusawazisha kupitia Carolyne Simiyu kwenye patashika iliyosakatiwa uwanjani fedha Nairobi.

”Mambo siyo mazuri kwetu maana hadi sasa tunasaka mfadhili lakini tunaendelea kujitahidi na kuwapiga breki wapinzani wetu,” kocha wa Mukuru Talent Academy, Amos Abong’o aliambia Taifa Leo Dijitali huku akisema wamepania kupigana kwa udi na uvumba kusaka tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi Kuu (KWPL) msimu ujao.

Mukuru Talent Academy iliteleza na kujiongezea alama kufuatia matokeo hayo huku ikijivunia kuponda MTG kwa mabao 3-2 wiki tatu zilizopita.

Ndani ya mechi mbili, Joyce Lina alipiga ‘hat trick’ naye Mercyline Mwalimu alitingia MTG bao moja na kuisaidia kuandikisha alama nne.

Nao Emmaculate Adhiambo na Hannah Mbithe walifanikiwa kucheka na nyavu mara moja kila mmoja na kusaidia Limuru Starlets kwenye mchezo huo kuvuna alama moja.

Nayo Joy Love ilikubali kulala kwa mabao 2-0 mbele ya Mombasa Olympic baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 na Sunderland Samba kwenye ufunguzi.