Michezo

Mtihani kamili wa Man United ni dhidi ya Spurs – Phil Jones

January 8th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MLINZI wa Manchester United Phil Jones amekiri kwamba mechi kati yao na Tottenham Hot Spurs ugenini Jumapili Januari 13 ndiyo itakuwa kipimo kamili kwa timu hiyo tangu kocha mpya Ole Gunnar Solskjaer achukue usukani.

Tangu waagane na kocha wao wa zamani Jose Mourinho baada ya kichapo cha 3-1 mikononi mwa Liverpool ugenini Anfield, Manchester United maarufu kama ‘The Red Devils’ wameshinda mechi zote tano zilizofuatia. Hata hivyo ushindi huo umekuwa dhidi ya timu dhaifu zilizoko katika nafasi ya chini kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza(EPL).

“Mechi dhidi ya Spurs itakuwa mtihani mkubwa kwetu na tisho la kusitisha ushindi wetu katika mechi tano mfululizo. Tupo katika fomu nzuri kwa sasa na tumeweza kubatilisha zimwi la matokeo mabaya tuliyokuwa tukisajili awali,” akasema Jones.

Ingawa hivyo, difedha huyo kibonge amekiri kwamba Spurs pia wapo katika fomu ya kutisha na watafanya kila juhudi kumzuia mshambulizi matata Harry Kane dhidi ya kutamba.

Spurs kwa sasa wapo katika nafasi ya tatu kwa alama 48, sita nyuma ya viongozi wa ligi Liverpool na mbili nyuma ya mabingwa watetezi Manchester City.