Mtihani mgumu kwa Arsenal ugenini Etihad

Mtihani mgumu kwa Arsenal ugenini Etihad

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MABINGWA watetezi Manchester City watalenga kuongeza masaibu ya Arsenal ugani Etihad kwenye Ligi Kuu hii leo Jumamosi katika siku ambayo pia Liverpool na Chelsea watapimana ubabe uwanjani Anfield.

City ya kocha Pep Guardiola imebwaga Arsenal inayotiwa makali na mwanafunzi wa zamani wa Guardiola, Mikel Arteta, katika mechi tatu zilizopita katika mashindano yote.

Haijapoteza dhidi ya Arsenal katika mechi 11 mfululizo ligini. Vijana wa Guardiola wamezoa ushindi mara nane mfululizo ligini kwa jumla ya mabao 19-1.

City inayoshikilia nafasi ya tisa ina motisha baada ya kurarua Norwich 5-0 kupitia mabao ya Tim Krul (alijifunga), Jack Grealish, Aymeric Laporte, Raheem Sterling na Riyad Mahrez wikendi iliyopita.

Guardiola atakosa huduma za kiungo stadi Kevin De Bruyne anayeuguza bado jeraha.

Makinda Phil Foden na Ferran Torres na kiungo mbunifu Grealish ni baadhi ya wachezaji matata kambini mwa City ambao Arsenal italazimika kuwa makini nao inapotafuta kukwepa kichapo cha tatu mfululizo ligini.

Wanabunduki wa Arsenal walicharazwa 2-0 na Brentford na Chelsea katika michuano miwili yao ya kwanza ligini. Walipata motisha walipokung’uta West Brom kutoka Ligi ya Daraja ya Pili 6-0 kwenye Kombe la Carabao katikati mwa wiki na wanatarajiwa kuwa na mori ya kutafuta matokeo mema licha ya kibarua kigumu kinachowakabili.

Nambari mbili kutoka mkiani Arsenal ilizamisha West Brom kupitia mabao ya Pierre-Emerick Aubameyang (matatu), Nicolas Pepe, Bukaya Saka na Alexandre Lacazette. Saka alipata jeraha la goti katika mchuano huo.

Arteta, ambaye alihudumu kama naibu wa Guardiola ugani Etihad kabla ya kujiunga na Arsenal, atawategemea zaidi washambuliaji Aubameyang na Lacazette kutafuta magoli na kiungo mbunifu Martin Odegaard.

Rekodi ya Arsenal kutopoteza michuano mitatu mfululizo ya kwanza kwenye Ligi Kuu tangu msimu 1954-1955 itakuwa hatarini leo.Nambari mbili Chelsea na nambari tatu Liverpool walishinda mechi zao mbili za kwanza.

Msimu uliopita, Chelsea ya kocha Thomas Tuchel ilipigwa 2-0 ugani Stamford Bridge mwezi Septemba 2020 kabla ya kulipiza kisasi 1-0 dhidi ya vijana wa Jurgen Klopp ugani Anfield mwezi Machi 2021.

Hii leo, macho yatakuwa kwa washambuliaji matata Romelu Lukaku (Chelsea) na Mohamed Salah (Liverpool) pia kiungo N’Golo Kante na beki Virgil van Dijk.

Ratiba:

Agosti 28 – Manchester City vs Arsenal (2.30pm), Newcastle vs Southampton (5.00pm), Brighton vs Everton (5.00pm), West Ham vs Crystal Palace (5.00pm), Norwich vs Leicester (5.00pm), Aston Villa vs Brentford (5.00pm), Liverpool vs Chelsea (7.30pm);

Agosti 29 – Burnley vs Leeds (4.00pm), Tottenham vs Watford (4.00pm), Wolves vs Manchester United (6.30pm).

You can share this post!

Madiwani wataka kupewa bunduki ‘kupambana’ na polisi

FATAKI: Raha jipe mwenyewe dada, siache vigezo vya jamii...