Michezo

Mtihani mgumu kwa Ulinzi ikivaana na Tusker FC ligini

March 20th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FATAKI zinatarajiwa leo Jumatano kulipuka uwanjani Ruaraka wakati Tusker FC watakapokuwa wenyeji wa wanajeshi wa Ulinzi Stars katika mechi ya Ligi Kuu ya KPL.

Chini ya kocha Robert Matano, Tusker watajibwaga ugani wakipania kusajili ushindi utakaowapaisha hadi nafasi ya saba jedwalini.

Kufikia sasa, mabingwa hao mara 11 wa taji la KPL wanashikilia nafasi ya tisa kwa alama 22 baada ya kupiga jumla ya michuano 16.

Ni alama moja pekee inayowatenganisha Tusker na Ulinzi Stars ambao kwa sasa wanalenga kujikweza pazuri katika jedwali la KPL baada ya kubanduliwa na SS Assad kwenye kivumbi cha SportPesa Shield muhula huu.

Ushindi kwa Ulinzi Stars wanaotiwa makali na kocha Dunstan Nyaudo, utawapa hamasa zaidi ya kuhimili makali ya Gor Mahia watakaokuwa wageni wao mwishoni mwa wiki hii uwanjani Afraha, Nakuru.

Mechi hiyo ambayo awali ilikuwa imeratibiwa kutandazwa mnamo Machi 3, iliahirishwa hadi Machi 6 kabla ya kusogezwa upya ili kupisha kampeni za kimataifa za CAF zinazoshirikisha Gor Mahia.

Baada ya kumenyana na Tusker hii leo Jumatano, Ulinzi Stars ambao ni wafalme mara nne wa KPL, watashuka dimbani kupimana ubabe na Gor Mahia kabla ya kuwaalika mabingwa wa 2006 SoNy Sugar mnamo Machi 27.

Nafasi ya pili

Gor Mahia ambao Jumanne walikuwa wenyeji wa Kenpoly katika mechi ya SportPesa Shield uwanjani Kasarani, kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 32 sawa na Bandari ambao zaidi ya kuwa na mabao machache, pia wamecheza mechi moja zaidi.

Kwingineko, Nzoia Sugar watachuana na Zoo Kericho mjini Bungoma huku Bandari wakipania kuendeleza ukatili wao dhidi ya SoNy Sugar uwanjani Awendo.

Nzoia wanashikilia nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 20, tano zaidi kuliko Zoo ambao wananing’ia pembamba mkiani baada ya kusajili ushindi mara tatu, kuambulia sare mara sita na kupoteza jumla ya mechi nane kati ya 17 zilizopita.

Kwa upande wao, SoNy Sugar wanafunga orodha ya saba-bora kwa alama 25 huku pengo la pointi saba likitamalaki kati yao na Bandari.

Mwishoni mwa wiki jana, Vihiga United waliruka hadi nafasi ya 13 nao Kakamega Homeboyz wakapaa hadi nafasi ya nane baada ya kuanza mechi za mkondo wa pili za KPL kwa matao ya juu.

Vihiga ina alama 18, moja mbele ya Chemelil Sugar ambao wanawazidi Posta Rangers na AFC Leopards kwa pointi moja vilevile.