Mtihani mgumu unaosubiri Mkenya Onyango kuingiza wanaraga wa Uganda kwenye Olimpiki

Mtihani mgumu unaosubiri Mkenya Onyango kuingiza wanaraga wa Uganda kwenye Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanaume inayonolewa na Mkenya Tolbert Onyango, imetiwa katika kundi moja na wakali Ufaransa kwenye mashindano ya mwisho ya kufuzu kushiriki Olimpiki mnamo Juni 19-20 mjini Monaco.

Mbali na mabingwa hao wa duru ya Raga ya Dunia ya Paris Sevens mwaka 2005 wanaopigiwa upatu kutesa katika mashindano hayo ya mataifa 10, Waganda pia watakabiliana na Hong Kong, Chile na Jamaica katika Kundi A.

Vijana wa Onyango wako nchini Afrika Kusini wakati huu kwa kambi ya mazoezi na mashindano ya kujipima nguvu dhidi ya Kenya, Afrika Kusini na Zimbabwe na timu nyingine tatu kutoka Afrika Kusini.

Watalazimika kufanya kazi ya ziada kupata tiketi moja ambayo iko mezani kutoka mashindano hayo kwenye Olimpiki.

Kundi B linaleta pamoja mataifa ya Samoa, Ireland, Tonga, Zimbabwe na Mexico.

Ufaransa, Samoa na Ireland zinashiriki duru zote za Raga ya Dunia. Hii inaweza kuashiria kuwa kundi la kwanza ni rahisi kidogo ikilingalishwa na kundi la pili.

Droo ya mchujo huo wa mwisho wa kuingia Olimpiki ilifanywa mjini Monaco mnamo Jumanne. Ile ya wanawake pia imekamilishwa ambapo Urusi, Argentina, Mexico na Samoa zitapepetana katika Kundi A, Papua New Guinea, Kazakhstan, Jamaica na Tunisia ziko Kundi B nazo Ufaransa, Hong Kong, Colombia na Madagascar zinakamilisha kundi la mwisho.

  • Tags

You can share this post!

Jubilee haitambembeleza Kuria, atatimuliwa chamani –...

Kenya Power yazidi kumulikwa kwa utepetevu