Habari Mseto

Mtindo wa kutimua manaibu jaji mkuu wanawake wakejeliwa

August 30th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KUNA njama za kuwadhulumu na kuwatimua kazini majaji wanawake wanaoteuliwa kuwa Naibu wa Jaji Mkuu (CJ), mahakama inayoamua kesi za ufisadi ilifahamishwa Jumatano.

Wakili Dkt John Khaminwa anayemwakilisha Naibu wa Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mwilu alisema majaji wawili waliomtangulia kuhudumu katika wadhifa huo walimtumuliwa afisini kwa njia sisizofurahisha kamwe.

“Inaonekana kuna watu wanaofanya mashauri mahala jinsi watafanyia idara ya mahakama mabadiliko kwa kuwang’oa DCJ,” alisema Dkt Khaminwa.

Akimweleza hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za  ufisadi kuwa  idara ya mahakama inakabiliwa na hali ya hatari Dkt Khaminwa alisema waliomtangulia Jaji Mwilu kuwa DCJ , Nancy Baraza na Kalpana Rawal waling’olewa afisini kwa njia zisizoridhisha.

“Jaji Baraza alimtimuliwa kwa kumchuna bawabu pua katika Village Market naye Jaji Rawal alimtimuliwa asimridhi aliyekuwa CJ Willy Mutunga kwa madai alikuwa amehitimu umri wa miaka 70 ilhali akiajiriwa alikuwa ameelezwa atastaafu akiwa na umri wa miaka 74,” alisema Dkt Khaminwa.

“Sasa ni zamu ya  Jaji Mwilu anayedaiwa alifanya makosa kupokea mkopo kutoka kwa benki,” alisema Dkt Khaminwa.

Dkt Khaminwa alimweleza hakimu mkuu Bw Lawrence Mugambi kuwa kila afisa wa idara ya mahakama anaishi kwa woga sasa kwa vile hawajui atakayefuata atakuwa nani akiongeza , “anaweza kuwa ni hakimu ama jaji.”