Habari za Kitaifa

Mtindo wa pesa kumezwa na mishahara badala ya maendeleo wahamia kwa kaunti


MISHAHARA na marupuru yanatarajiwa kumega sehemu kubwa ya mapato ya kaunti, kulingana na bajeti za 2024/2025 zilizopitishwa na kaunti mbalimbali.

Katika mwaka huu wa fedha, baadhi ya kaunti zinalenga kutumia zaidi ya asilimia 70 ya bajeti kwa matumizi ya kawaida, na mgao mdogo sana kwa miradi ya maendeleo.

Haya yanajiri miezi kadhaa baada ya Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakang’o kuonya serikali za kaunti dhidi ya kupaa kwa viwango vya ulipaji mishahara na marupurupu.

Katika ripoti yake iliyoangazia miezi tisa ya kwanza ya Mwaka wa Fedha wa 2023/2024, Bi Nyakang’o alifichua kuwa ni kaunti za Narok na Kilifi pekee ambazo zimeweza kuweka ukomo wa matumizi ya fedha kwa mishahara chini ya asilimia 35 ya matumizi yote.

Katika ripoti ya matumizi ya miezi tisa, mdhibiti huyu wa bajeti alitilia mkazo kuwa kaunti hutumia pesa kwa mishahara ya wafanyakazi kuliko inavyotarajiwa kisheria.

“Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma ya 2012, inataka angalau asilimia 30 ya bajeti itengwe kwa ajili ya mipango ya maendeleo. Ninazitaka kaunti zidhibiti bili zinazoongezeka,” alisema Bi Nyakang’o.

“Kaunti nyingi zimelazimika kupambana na ada kubwa za mishahara zinazomega zaidi ya nusu ya Bajeti za kila mwaka za kaunti. Kwa hivyo, hutatiza shughuli za maendeleo. Wengi wa magavana wapya hawajaweza kuanzisha miradi ya maendeleo kutokana na ada kubwa zinazozidi kuongezeka.”

Ubadhirifu mkubwa wa pesa

“Kuna ubadhirifu mkubwa sana wa fedha katika kaunti kumudu bili zinazozidi kupanda. Baadhi ya kaunti hutumia asilimia 75 ya fedha kulipa mishahara huku asilimia 25 ikitumika kwa maendeleo,” Bi Nyakang’o aliongeza.

Wadhibiti wawili wakuu wa utumizi wa fedha za umma wanaorodhesha malipo kinyume cha sheria, wafanyakazi wengi na malipo ya kiholela kuwa visababishi vikubwa vya ubadhirifu wa fedha.

Na katika mwaka huu wa kifedha, Kaunti za Migori, Murang’a, Taita Taveta, Kakamega, Narok na Trans Nzoia hazina budi ila kuendelea kuzongwa na hali hizi za matumizi ya fedha.

Katika kaunti ya Murang’a, kati ya bajeti ya Sh10.46 bilioni iliyopitishwa wiki jana na bunge la kaunti kwa mwaka wa kifedha wa 2024-2025, Sh3.15 bilioni zimetengwa kwa maendeleo na Sh7.29 bilioni kwa matumizi ya kawaida.

Haya ni kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti na Matumizi, Charles Machigo.

Na katika kaunti ya Narok, mwanachama wa kamati kuu ya kaunti, anayesimamia Fedha David Ole Muntet, amewasilisha bajeti ya Sh15.7 bilioni kwa mwaka wa kifedha wa 2024/2025.

Kulingana na Bw Muntet, asilimia 34 ya bajeti imetengwa kwa malipo ya mishahara ya wafanyikazi, asilimia 33 itatumika katika shughuli za kaunti, huku asilimia 33 ikipangiwa maendeleo.

Bunge la kaunti ya Kakamega liliidhinisha bajeti ya Sh17.8 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.

Kati ya fedha hizo, Sh11.9 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ambayo ni sawa na asilimia 66.7 huku Sh5.9 bilioni zikitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikiwa ni asilimia 33.3 ya bajeti nzima.

Mapato ya wafanyakazi yatachukua jumla ya Sh6,857,312,177 ya matumizi ya kawaida, huku oparesheni na ukarabati ukitumia Sh 5 bilioni.

Huko Migori, wawakilishi wadi wameidhinisha bajeti ya Sh10.386 bilioni kwa mwaka huu wa kifedha.

Hata hivyo, matumizi ya kawaida yatameza takriban Sh6.9 bilioni za bajeti kwa asilimia 66.9, na kusalia Sh3.4 bilioni pekee kwa maendeleo.

Vile vile, huko Trans Nzoia, bunge limeidhinisha bajeti ya Sh9.9 bilioni huku kaunti ikitenga Sh6 bilioni kwa matumizi ya kawaida na Sh3.9 bilioni kwa maendeleo.

Katika kaunti ya Taita Taveta, madiwani wamepitisha bajeti ya Sh8.3 bilioni huku matumizi ya kawaida yakichukua sehemu kubwa ya asilimia 67.4 ya mgao huo.

Katika mdahalo wa Mswada wa Ugavi Rasilimali wa Kaunti 2024, Wajumbe wa Bunge la Kaunti walikerwa na matumizi ya bajeti kwa ajili ya ada za kawaida iliyofika asilimia 53.

Kadhalika, katika kaunti ya Kiambu, Gavana Kimani Wamatangi atatumia kiasi kikubwa cha bajeti ya kima cha  Sh23.5 bilioni kulipa mishahara na marupurupu.

Nayo kaunti ya Nyeri iliyoidhinisha bajeti ya Sh5.8 bilioni itatumia Sh8.7 bilioni kwa matumizi ya kawaida, huku Sh2.8 bilioni zikifadhili maendeleo.

Kiasi kilichotengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kinawakilisha asilimia 33.04 ya bajeti yote huku mishahara na marupurupu yakimega asilimia 66.95.