Habari Mseto

Mtoto afariki baada ya kamba aliyochezea kukwama shingoni

December 12th, 2018 1 min read

Na Benson Amadala

HALI ya mshangao imekumba kijiji kimoja katika Kaunti ya Kakamega baada ya mwanafunzi wa Darasa la Nne kufariki wakati kamba aliyokuwa akichezea kukwama kwenye shingo yake.

Mvulana huyo, ambaye alitambuliwa kama Winston Litiema alisemekana kufunga kamba hiyo katika mojawapo ya mbao za nyumba yao Jumatatu jioni na kuanza kuichezea.

Babake, Kennedy Isalamba alikuwa ameenda kanisani mkasa huo ulipotokea.Mkasa huo ulitokea katika kijiji cha Mulundu, Kaunti Ndogo ya Kakamega Mashariki.

Bw Isalamba amekuwa akiishi na wanawe wawili nyumbani kwake.

Mvulana huyo alifariki baada ya kamba hiyo kumfinya shingoni, hivyo kumzuia kupumua vizuri.

Kifo hicho cha kusikitisha kiliripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Shisasari. Mkuu wa Polisi katika eneo hilo Robert Makau alisema tayari wameanza uchunguzi kubaini kiini halisi cha kifo hicho.

Nduguye marehemu alisema kwamba alikuwa akiosha vyombo wakati aliona mwili wa kakake ukining’inia.