Habari Mseto

Mtoto afariki yaya akitazama runinga

January 8th, 2019 2 min read

PETER MBURU na JOSEPH OPENDA

MWANAMKE mmoja ambaye alikuwa yaya wa wakili mjini Nakuru anasakwa na polisi kufuatia kisa ambapo mtoto wa chini ya mwaka mmoja aliyekuwa akimlea aliaga dunia kwa kunyongwa na chakula, wakati yaya huyo alikuwa akitazama runinga.

Iliripotiwa kuwa mnamo Desemba 14 mwaka uliopita, Bw Steve Opar, wakili, na mkewe Wendy Audrey walimwacha mtoto wao mvulana na msaidizi wao wa nyumbani katika mtaa wa St Mary’s kama kawaida yao na wote wakaenda shughuli zao.

Bw Opar alikuwa mjini Nyahururu katika kaunti ya Laikipia alipopokea simu mwendo wa saa kumi na moja jioni kutoka kwa jirani kuwa mwanawe alikuwa katika hali mbaya.

“Alisema kuwa mtoto ‘Jayden’ alikuwa anaelekea kufa kwa kunyongwa na chakula. Nilimwambia amkimbize hospitalini nikiwa nimechanganyikiwa kwani mtoto huyo alikuwa kila kitu kwangu. Pia nilimpigia mke wangu na kumwambia akimbie hospitalini,” akasema Bw Opar.

Lakini alipofika hospitalini, mkewe alipata tayari mtoto ameaga dunia. “Hata sikupata fursa ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa mara ya kwanza kwani hakuwa amefikisha mwaka. Ulikuwa wakati mgumu sana,” akasema Bi Wendy.

Lakini waliporejea nyumbani, hawakumpata kijakazi wao wa miaka 23, ndipo wakaingiwa na shauku kuhusu sababu yake ya kutoroka. Alikuwa ameajiriwa miezi miwili tu iliyotangulia.

Ni jirani yao, Bi Naomi Wambui ambaye aliwafahamisha wazazi hao kuwa pia naye alipata habari kutoka kwa nduguye wakili huyo kuwa hali ya mtoto haikuwa nzuri, ijapokuwa kijakazi alikuwa akitazama runinga.

“Nilikimbia ndani ya nyumba na kumpata kijakazi akitazama runinga. Nilipomuuliza alipo mtoto, aliashiria upande wa chumba cha kulala na nilipoingia nilishtuka kumpata mtoto akigaagaa chali,” akasema.

Polisi sasa wameanza uchunguzi baada ya wanandoa hao kupiga rip[oti katika kituo cha Teacher’s mjini Nakuru.

Bi Wendy alidai kuwa alikuwa akitafuta kijakazi mwingine baada ya kubaini kuwa kila huyo alipombeba mtoto, alikuwa akianza kulia.

Mtoto huyo alizikwa mnamo Desemba 18, japo wanandoa hao bado wanaomboleza na wanaomba yeyote aliye na habari kuhusu alipo kijakazi huyo kupiga ripoti kwa kituo chochote cha polisi.