Mtoto aibwa mchana punde baada ya kuzaliwa

Mtoto aibwa mchana punde baada ya kuzaliwa

Na BRIAN OJAMAA

HALI ya sintofahamu imekumba familia moja katika eneo la Machinjoni, eneobunge la Kimilili katika Kaunti ya Bungoma, baada ya mtoto wao kutoweka mara baada ya kuzaliwa katika hospitali ya Kimilili.

Mtoto huyo alitoweka Jumatano mchana – hali ambayo imeacha familia hiyo na mashaka tele. Mama wa mtoto huyo, Joy Nakhumicha, alipelekwa na mumewe Joseph Sirengo hospitalini hapo kujifungua Jumanne.

Baada ya kujifungua, mtoto huyo anadaiwa kukabidhiwa kwa mwanamke mwingine aliyedhaniwa kuwa mmoja wa jamaa zake.

Mwanamke huyo aliyejifanya kuwa dadaye alitoweka na mtoto huyo kabla ya Bi Nakhumicha kutoka kwenye chumba cha kujifungua ambapo alikuwa amemzaa kwa njia ya upasuaji. Muuguzi aliyemsaidia Nakhumicha kujifungua alidai kuwa alimpa jamaa yake mtoto.

Lakini jamaa zake walioandamana naye hospitalini walishikilia kuwa hawakuona mtoto huyo wa kiume. Bi Nakhumicha aliambia wanahabari hospitalini hapo kwamba alijifungua mtoto wa kiume aliyekuwa buheri wa afya lakini hakuweza kuwa naye kitandani kwani alikuwa akihisi maumivu makali.

“Kifungua mimba wangu ni msichana na niliomba sana Mungu anipe mtoto wa pili wa kiume na alisikia maombi yangu. Nashangaa kuambiwa kwamba hapatikani,” akasema Bi Nakhumicha. Mkuu wa hospitali hiyo Bw David Shivachi alikiri kuwa mtoto huyo alitoweka katika hali ya kutatanisha.

Bw Shivachi alisema hospitali tayari imeripoti kwa polisi na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) na tayari uchunguzi unaendelea. Alisema maafisa wa uchunguzi sasa wanategemea kamera za CCTV zilizo katika majengo ya benki ya karibu na hospitali hiyo ili kutambua mwanamke aliyeiba mtoto huyo.

Alisema kamera za CCTV hospitalini hapo zimeharibika.

You can share this post!

UGUMU WA MAISHA KUZIDI OKTOBA

Raila kuhudhuria uzinduzi wa chama cha PAA