Kimataifa

Mtoto ajiua kwa kusimangwa kuwa shoga

August 28th, 2018 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

MVULANA mchanga kutoka Marekani alijiua Alhamisi, siku nne baada ya kuanza mwaka mpya wa shule, baada ya kuhangaishwa na wenzake alipokiri mbele yao kuwa shoga.

Mamake Jamel Myles, mvulana wa miaka tisa alisema mwanaye alijiangamiza baada ya wenzake shuleni ambao hawakukubaliana na hali yake ya mapenzi kuanza kumtesa shuleni.

Mtoto huyo alipatikana akiwa amefariki nyumbani kwao eneo la Denver Alhamisi. Alikuwa ameanza masomo ya darasa la nne katika shule ya Joe Shoemaker Elementary, Jumatatu iliyopita.

“Ilimchukua siku nne pekee shuleni, nikuwaza tu ambacho wanawezakuwa walimwambia,” Bi Leia Pierce, mamake akasema.

“Mtoto wangu alijiua, hakuhitaji kukumbana na haya, alipenda kumfurahisha kila mtu hata wakati yeye hakuwa na furaha, napenda kumwona hai tena,” akasema mama huyo.

Bi Pierce alisema mwanawe alipokiri mbele yake kuwa alikuwa shoga alionekana kuwa mwenye woga mwingi.

“Nilidhani kuwa alikuwa akifanya mzaha hivyo sikushughulika kwa kuwa nilikuwa nikiendesha gari. Nilimwambia bado nampenda,” mama huyo akasema.

Alisema mwanaye aliamua kuwaeleza wenzake shuleni kuhusu hali yake kwa kuwa tayari alikuwa amejikubali.