Mtoto Asome: Wanafunzi 50 kujiunga na shule baada ya kupokea ufadhili

Mtoto Asome: Wanafunzi 50 kujiunga na shule baada ya kupokea ufadhili

NA FARHIYA HUSSEIN

ZAIDI ya wanafunzi 50 kutoka kaunti ya Mombasa waliopata alama kuanzia 350 wataweza kujiunga na shule za upili baada ya kupokea ufadhili.

Vijana hao sasa wataweza kuendelea na masomo ya shule ya upili baada ya Seneta Maalum Bi Miraj Abdillah kutenga shillingi milioni moja kupitia mradi wa Mtoto Asome.

“Nina furaha siku ya leo. Wazazi wangu walikuwa hawajui wataanzia wapi kwa vile nilikuwa nimeitwa shule upande wa Muranga, lakini kupitia ufadhili huu nitajiunga na shule ilioko Malindi,” alisema mmoja wa wanafunzi Dennis Musyoka aliyepata alama 366 katika KCPE.

Seneta Maalum Bi Miraj Abdillah ametenga Sh1 milioni kupitia mradi wa Mtoto Asome ili wanafunzi waliopata alama kuanzia 350 wajiunga na shule za upili. PICHA | FARHIYA HUSSEIN

Mwenzake Rabiya Jabir aliyeitwa shule ya upili ya wasichana ya Mama Ngina alisema,”Huu mradi ni baraka tele kwangu. Babangu alikuwa hana wa kumlilia. Ninashukuru nitaweza kuendelea na masomo yangu.”

Seneta Maalum Abdilla alisema mradi huo unalenga watoto wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini ambao walifanya vyema katika mtihani wao wa Darasa la Nane.

“Watoto wenye alama ya 350 kutoka shule za mabanda na wale wameitwa shule za kimataifa, walikuwa wanatafutiwa shule za huku chini kwa vile hawana uwezo wa kujiunga na zile walizoitwa,” alisema Bi Abdillah.

Bi Abdillah alisema mradi huo unapanga kutatua changamoto wanazopitia wazazi na watoto katika ufadhili wa masomo.

“Ikiwa tutatua suala la elimu katika magatuzi yetu basi tutatua masuala ya magenge ya uhalifu na mimba za mapema hapa Mombasa. Mpango huu pamoja na kupigana na masuala ya mzunguko wa umaskini ambao imekuwa donda sugu hapa pwani,” alieleza Bi Abdillah.

Seneta huyo alisema aliafikia maamuzi hayo baada ya kugundua wanafunzi wengi wanakosa ufadhili wa basari zinazotolewa na mashirika mbalimbali na benki.

“Tulitoa mawasiliano na kwa wiki moja tumeweza kupata maombi zaidi ya 50 kutoka kwa watoto ambao wana alama za juu kwenye mtihani wao wa Darasa la Nane,” alisema Bi Abdillah huku akiwarai wanafunzi hao kutia bidii masomoni akiahidi kuwalipia karo zao mpaka wakamilishe masomo ya Kidato cha Nne.

Mzazi mmoja, Bw Stephen Ngalo alitoa shukrani zake akielezea changamoto alizopitia katika kutafuta bursary kupitia NG-CDF.

Seneta Maalum Bi Miraj Abdillah ametenga Sh1 milioni kupitia mradi wa Mtoto Asome ili wanafunzi waliopata alama kuanzia 350 wajiunga na shule za upili. PICHA | FARHIYA HUSSEIN

Katibu wa Mashule ya Mabanda Bw Juma Athman alithibitisha kupokea kwa Sh1 milioni zitakazosimamia ufadhili wa wanafunzi waliopita mtihani wa Darasa la Nane na kukosa namna.

“Suala la elimu si la mzaha. Viongozi wengi wanajitetea kutokana na CDF ilhali bado watoto wengi wanakosa kujiunga na shule na wengi ndoto zao za kuendelea na masomo zao hukatizwa,” alisema Bw Athman.

  • Tags

You can share this post!

DOMO: Mtu asiniambie kuhusu mapenzi

KASHESHE: ‘Nameless alinichanua’

T L