Habari

Mtoto azaliwa miaka minne baada ya wazazi wake kuangamia ajalini

April 12th, 2018 2 min read

MASHIRIKA na CHARLES WASONGA

MIAKA minne baada ya mke na mume kufariki gari lao lilipohusika katika ajali, mtoto wao alizaliwa na mama mbadala kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini China.

Mtoto huyo aliyepewa jina, Tiantian, alizaliwa nchini China na mwanamke wa asili ya nchi ya Laos, gazeti la The Beijing News limeripoti.

Inasemekana kuwa nyanya na babu za mtoto huyo wamethibitisha kuwa na uhusiano naye, wa kinasaba, kupitia uchunguzi wa chembechembe za DNA.

Wanandoa hao, raia wa China, ambao walifariki mnamo 2013 walikuwa wamehifadhi viinitete (embryos) kadha kwa matumaini ya kupata mtoto kwa mbinu ya kisiasa, maarufu kama, “In vitro Fertilization” (IVF).

Hii ni kutokana na sababu kwamba mke hakuwa na uwezo wa kupata mimba kwa njia ya kawaida.

Baada ya ajali, wazazi wa wanandoa hao walijaribu mbinu zote kupitia njia za kisheria wakitaka waruhusiwe kutumia viinitete hivyo.

Mtoto huyo mvulana alizaliwa mnano Desemba 2017 na mama mbadala lakini gazeti la The Beijing News liliripoti kisa hicho wiki hii.

Gazeti hilo lilielezea jinsi kukosekana na kisa cha awali aina hiyo kiliwalazimu wazazi wa wanandoa hao kupitia visiki vya kisheria kabla ya mama huyo mbadala kuruhusiwa kubeba watoto hao tumboni mwake.

Ajali hiyo ilipotokea, viinitete hivyo vilikuwa vimehifadhiwa salama katika Hospitali ya Nanjing katika mazingira baridi zaidi ndani ya tangi la hewa ya Nitrojeni.

Mahakama ilitoa idhini ya wazazi wanne wa wanandoa hao kumiliki mayai hayo ambayo yalikuwa yameunganishwa kuzaa viinitete.

Kulingana na ripoti hizo, hamna kesi za awali za aina hiyo ambayo ingewaruhusu wazee hao kurithi viinitete vya wanao vilivyohifadhiwa.

 

Vizingiti

Changamoto nyingine iliyowakabiliwa na jinsi ya kupata mama mbadala. Kwa kuwa huduma hiyo imepigwa marufuku nchi China, walilazimika kuangazia ng’ambo na hatimaye wakatua nchini Laos ambako huduma hizo sio marufuku.

Shida nyingine iliyowakabili ni kwamba hakuna shirika la ndege lililokubali kusafirisha viinitete hivyo, hali iliyowalazimu kuvisafirishwa kwa barabara kwa siku nyingi.

Nchini Laos, kiinitete kimoja kiliwekwa ndani ya tumbo ya mama mbadala na mnamo Desemba 2017 mtoto mvulana alizaliwa.

Uraia wa mtoto huyo kwa jina Tiantian, ni changamoto nyingine ambayo wazee hao walikumbana nayo.

Kwa hivyo, ilibidi mama huyo kumzalia mtoto nchini China wala sio Laos, baada ya mama huyo kuingia humo (China) kama mtalii.

Kwa kuwa mtoto huyo hakuwa na wazazi, iliwalazimu wazee hao kupeana damu zao ili uchunguzi wa DNA ufanywe kubaini kuwa alikuwa mjukuu wao halisi na kwamba wazazi wake walikuwa raia halisi wa China.