Habari Mseto

Mtoto mchanga apatikana katupwa kando ya lori mjini Thika

September 19th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MTOTO mchanga alipatikana ametupwa na kutelekezwa kando ya lori.

Bawabu mmoja katika kituo cha petroli mjini Thika alisikia sauti ya mtoto mchanga naye kwa haraka alimjulisha mhudumu wa teksi ambaye alikuwa ameegesha gari lake hapo.

Ilikuwa ni mwendo wa saa kumi na moja za alfajiri mnamo Jumatano, ambapo dereva huyo kwa ujasiri alimpangusa mwili na kumfanyia huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka katika hospitali kuu ya Thika Level 5.

“Nilikuwa nimeegesha gari langu kando ya kituo cha petroli hapa mjini Thika. Baadaye niliitwa na bawabu mmoja akinieleza kuwa alimuona mtoto mchanga chini ya lori na alitaka usaidizi wangu,” alisema mhudumu wa teksi ambaye hakutaka jina lake lichapishwe.

Alisema alifanya juhudi kumhudumia mtoto huyo kadri ya uwezo wake, na baadaye alipiga ripoti kituo cha polisi ambako aliandikisha taarifa.

“Nilipokamilisha kuandika taarifa, niliandamana na polisi hadi hospitalini ambako tulikubaliwa kumweka huko ili achunguzwe zaidi.

Yuaendelea salama

Afisa mkuu wa hospitali hiyo Dkt Jackline Wangeci Njoroge, alisema baada ya kumkagua kiafya walipata ya kwamba anaendelea vyema na hakuwa na tatizo lolote mwilini.

“Tutaendelea kumkagua afya yake halafu baadaye tutamwasilisha katika kituo cha kuhifadhi watoto wadogo cha Thika Children’s Home ili aweze kupata malezi bora,” alisema Dkt Njoroge.

Alisema kulingana na ripoti wanazopata katika hospitali hiyo, kesi nyingi za watoto kutupwa zinaripotiwa mara tatu hivi kwa mwezi.

“Ninawashauri wasichana na wanawake wanaowatupa watoto wao kuzingatia upangaji wa uzazi ama wakichoka na watoto wao wawapeleke katika vituo vya kuhifadhi watoto,” alisema Dkt Njoroge.

Polisi wametoa mwito kwa wananchi kupiga ripoti ikiwa wana fununu kuhusu ni nani alimtupa mtoto huyo kando ya lori na kutoweka.

Idara hiyo tayari inaendeloea kufanya upelelezi ili kumpata aliyetekeleza unyama huo wa kumtupa mtoto malaika.