Habari Mseto

Mtoto wa miaka 2 anajisiwa, kunyongwa na kutupwa chooni

October 1st, 2018 1 min read

Na WAANDISHI WETU

POLISI katika eneo la Mang’u, eneobunge la Gatundu Kaskazini, wanachunguza mauaji ya mtoto msichana wa miaka miwili, ambaye mwili wake ulipatikana ndani ya shimo la choo alimotupwa baada ya kunajisiwa na kunyongwa.

Duru zilisema kuwa mtoto huyo alinajisiwa na kuuawa wakati familia yake ilipokuwa ikiandaa mazishi ya babu ya msichana huyo.

Katika Kaunti ya Lamu, mwanamume wa miaka 68 alikamatwa kwa kumuua kwa kumdunga kisu kijana wa miaka 25 kufuatia mzozo wa kifamilia.

Bw Omar Lola Hussein anadaiwa kumdunga kisu Bw Issa Hussein Shidho walipozozana wakati wakitafuna miraa kijijini Kiangwe, Kaunti Ndogo ya Lamu Mashariki.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Joseph Kanyiri, alisema mshukiwa tayari amekamatwa na anazuiliwa katika kituo cha polisi cha kisiwa cha Lamu akisubiri kupelekwa mahakamani.

Kwingineko, polisi katika eneo la Maara, Kaunti ya Tharaka Nithi wanamzuilia mwanaume kutoka kijiji cha Kianjuki anayeshukiwa kumuua ndugu yake mdogo jana kwa kumkatakata kwa upanga.

Afisa mkuu wa polisi wa eneo hilo Bw Johnston Kabusia, aliambia waandishi wa habari kuwa marehemu, Benson Musimi alikufa muda mfupi tu baada ya kushambuliwa na ndugu yake mkubwa Anthony Mwenda.

Ripoti za KALUME KAZUNGU, LAWRENCE ONGARO na ALEX NJERU