Mtoto wa tajiri ana nafasi nzuri maishani – Benki ya Dunia

Mtoto wa tajiri ana nafasi nzuri maishani – Benki ya Dunia

Na VALENTINE OBARA

MTOTO anayezaliwa katika familia maskini nchini hupata nafasi ndogo ya kujiimarisha kiuchumi kuliko yule anayezaliwa katika familia inayojiweza kimapato, ripoti imebainisha.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Benki ya Dunia inasema kwamba hali hii husababishwa sana na ukosefu wa sera bora ambazo zinaweza kutoa nafasi sawa kwa kila mwananchi kujiinua kimaisha.

Miongoni mwa mataifa 75 yaliyofanyiwa utafiti, Kenya iliorodheshwa kati ya 25 za mwisho pamoja na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), Mali, Malawi, Uganda, Nigeria, Africa Kusini, Colombia, Ecuador, Guatemala na Panama.

Ingawa watafiti walikiri kwamba mataifa 75 ulimwenguni ni machache kwa kutambua hali halisi ilivyo, walisema matokeo ya utafiti huo ni muhimu kwa mataifa mbalimbali yanayokua kiuchumi.

“Wazazi wote hutaka watoto wao wawe na maisha bora kuliko yao wenyewe, lakini maazimio ya watu wengi, hasa walio maskini, huzimwa na ukosefu wa nafasi sawa,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Dunia, Bi Kristalina Georgieva kwenye taarifa.

Ripoti hiyo iliyoandikwa na kikundi cha watafiti na wachanganuzi wakiongozwa na Ambar Narayan na Roy Van der Weide, ilisema wakati mwingi hali hii husababishwa na jinsi hakuna sera za kuleta usawa wa kimapato na elimu katika jamii.

Ili kubadili hali, ilipendekezwa kuwa mataifa yaunde nafasi sawa kwa minajili ya kuondoa changamoto zinazokumba watu binafsi na familia wanapojaribu kujiimarisha kiuchumi.

Ilibainika tofauti zilizopo huwa katika masuala kama vile kiwango cha elimu cha anayesimamia familia, eneo ambapo watu wanaishi (mjini au mashambani), utajiri wa familia, hali halisi ya mtoto na hali ya watu walio katika familia.

Hata hivyo, Kenya ilisifiwa kwa juhudi zake za kupambana na ukosefu wa usawa katika elimu kama njia ya kupitia kwa mipango ya kuangamiza minyoo kwa watoto na kupeana chakula bila malipo shuleni.

Itakumbukwa kuwa serikali pia huwekeza pakubwa katika elimu ya msingi bila malipo, kama njia ya kutoa nafasi sawa ya maendeleo katika jamii.

“Inafaa tuwekeze kwa watoto kutoka wakati wanapokuwa na umri mdogo ili wawe na siha njema na pia wapate elimu bora. Tuhakikishe kuna mazingara bora na salama katika jamii kwa watoto kukua, kuelimika na kujistawisha, na tuweke hali sawa ya kiuchumi kwa kutoa nafasi bora za ajira na kuboresha uwezo wa kimapato,” akasema Bi Georgieva.

Bali na haya, mpango wa serikali kupeana fedha kwa wazee pia ulitajwa kama mbinu bora ya kupunguza umaskini katika jamii.

You can share this post!

Hoteli motoni kwa kuzuia mwanamke kunyonyesha

Gavana atishia kupiga marufuku tuktuk

adminleo