Habari Mseto

Mtoto wetu ni malaika, wazazi wa Mugo wa Wairumu sasa wamtetea

November 7th, 2018 2 min read

Na STELLA CHERONO

WAZAZI wa mwanamume anayesakwa na polisi kwa kudhulumu wagonjwa na kuwatibu bila kibali, James Mugo Ndichu, maarufu Mugo wa Wairimu, jana walimtetea vikali mtoto wao dhidi ya madai kuwa ni mhalifu.

“Mugo ni mtoto wangu ambaye ninamwonea fahari kuu. Hata kama mtanitisha kwa bunduki kubwa nitamtetea tu hata mkiniua,” mamake Regina Wairimu Ndichu alieleza Taifa Leo jana nyumbani kwao Dagoretti, Kaunti ya Nairobi.

Wazazi hao walisema madai dhidi ya mtoto wao yanatokana na wivu kwa sababu ya ufanisi wake.

“Alipokuwa akifuzu udaktari alikuwa tayari ana kliniki yake, akaamua asifanye masomo ya nyanjani kama inavyotakikana na serikali. Nadhani hayo ndiyo makosa aliyofanya katika taaluma yake na kufanya watu wadhani hajafuzu,” wakasema Bi Wairimu na mumewe Simon Ndichu Ndongi.

“Alipokuwa akisomea udaktari Chiromo, Mugo alifanya kazi katika chumba cha maiti cha Chiromo na kupata fedha alizotumia kuanzisha kliniki yake,” akaongeza mamake.

Mugo anatafutwa na polisi kufuatia ufichuzi wa televisheni ya NTV baada ya kunaswa kwenye video akiwadhulumu wagonjwa kwenye kliniki mtaani Kayole ikiwemo kutoa wanawake mimba.

Mnamo 2015 alikamatwa na kushtakiwa kwa kumbaka mgonjwa mahututi lakini kesi yake ikatupwa baada ya mashahidi kukosa kujitokeza.

Alisema baada ya kisa cha 2015, Mugo aliacha kwenda kuwatembelea nyumbani, mkewe akatoroka na kliniki yake ikafungwa. “Ni wakati huo ambapo maisha yake yalibadilika. Njama ya maadui zake ilikuwa imefaulu. Anaweza kuwa na kasoro nyingi lakini madai dhidi yake yametiwa chumvi,” alisema babake.

Walisema mara ya mwisho kuwatembelea ilikuwa miezi mitatu iliyopita lakini hakukaa kwani tangu 2015 hawatembelei sana kutokana na aibu. Walieleza pia kuwa hawajui aliko, jambo linalowatia wasiwasi.

Wazazi wake jana walisisitiza kuwa madai yanayoendelezwa ni uongo mtupu, kwa kuwa hata majirani wana ushuhuda kuwa kijana wao ni mtu mzuri, ambaye amekuwa akiwatibu vizuri.

“Kila aliyetibiwa na mwanangu atakwambia kuwa alitoa huduma bora hata kushinda za kwenye hospitali kubwa. Uliza yeyote,” akasema Bw Ndichu.

Majirani walisema kabla ya ufichuzi wa 2015, alikuwa ameheshimika kijijini kama mtu mwerevu na mwenye bidii.

Mamake anaamini kuwa washindani wa mwanawe huenda waliungana na kula njama ya kumwangamiza kitaaluma kutokana na “huduma bora” ambazo amekuwa akiwapa wateja wake.

“Hao wanaomsingizia uongo wanasema mwanangu hajasoma Chuo Kikuu cha Nairobi ilhali tulihudhuria hafla ya kufuzu kwake Disemba 10, 2000. Alifuzu na shahada kutoka Shule ya Matibabu ya Chuo Kikuu cha Nairobi,” akasema Bi Wairimu, huku akionyesha picha za Mugo siku ya kufuzu.

Alisema amekuwa na urafiki mkubwa na mwanawe, na kwamba hiyo ndiyo sababu akachagua kujiita ‘Mugo wa Wairimu’.

Alieleza kuwa mwanawe alisomea katika shule ya Gitiba Primary kisha Dagoretti High kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi

Kufikia Jumatano jioni polisi walikuwa bado wanamtafuta.