Michezo

MTU AKABWA: Ujerumani yajuta kukabwa na Argentina

October 11th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

DORTMUND, Ujerumani

KIKOSI cha majaribio cha Ujerumani kilikubali nyavu zake kuchanwa mara mbili Jumatano na timu ya Argentina iliyokosa supastaa Lionel Messi katika mechi ya kirafiki ilitotamatika 2-2 jijini Dortmund.

Ujerumani iliongoza kipindi cha kwanza 2-0 kupitia mabao ya Serge Gnabry na Kai Havertz, lakini Lucas Alario alibadilisha mechi alipojaza nafasi ya Paulo Dybala katika dakika ya 62.

Mshambuliaji huyu wa Leverkusen alirejesha bao moja na kisha kusaidia Lucas Ocampos kusawazisha katika dakika za lala-salama dhidi ya timu ya Ujerumani iliochezesha wachezaji wanne wapya.

Wachezaji wa Freiburg, beki Robin Koch, ambaye alijumuishwa kikosini Jumatatu na mshambuliaji Luca Waldschmidt walianza mechi hiyo.

Licha ya wachezaji 14 kujiondoa kutokana na ugonjwa ama jeraha, Ujerumani iliridhisha mapema dhidi ya Argentina iliyokuwa bila wachezaji nyota Messi, Sergio Aguero na Angel di Maria.

Huku Messi akitumikia marufuku kutokana na matamshi aliyonena katika Copa America, Dybala alishirikiana na Lautaro Martinez katika safu ya mbele ya Argentina.

Mechi hii haikuwa tofauti na marudiano ya fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 2014, ingawa beki wa Manchester United Marcos Rojo ndiye alikuwa amesalia katika kikosi cha Argentina kilichopoteza 1-0 dhidi ya Ujerumani mjini Rio de Janeiro.

Rojo alishirikiana na Nicolas Otamendi wa Manchester City katika safu ya ulinzi ya Argentina, iliyovuja mapema.

Wiki moja baada ya kufungia Bayern Munich mabao manne dhidi ya Tottenham, Gnabry aliweka Ujerumani kifua mbele 1-0 dakika ya 15.

Winga huyu alitumia kasi yake ya kutisha vyema baada ya kuadhibu Angel Correa alipopoteza mpira. Alichenga mabeki wa Argentina kabla ya kusukumia kipa Augustin Marchesin shuti ambalo lilijaa wavuni.

Rojo alipopoteza mpira kwa Gian-Luca Waldschmidt, Gnabry aligeuka kuwa mchangiaji wa pasi iliyofungwa na Havertz katika dakika ya 22.

Walishwa kadi za manjano

Dalili za Argentina kuanza kukata tamaa ilianza kuonekana wachezaji wake Otamendi na Rodrigo de Paul walipolishwa kadi za manjano kwa kuchezea visivyo Julian Brandt na Gnabry, mtawalia.

Hata hivyo, Argentina ilikuwa na kipindi kizuri katika dakika 45 za mwisho, kuanzia wakati kocha Lionel Scaloni alipoingiza Alario katika nafasi ya Dybala.

Mshambuliaji huyo wa Leverkusen alidhihirisha nguvu zake hewani na kumwaga kipa Marc-Andre ter Stegen dakika nne baadaye kupitia kichwa chake.

Wageni walisawazisha wakati Alario alimmegea pasi safi Ocampos. Ocampos, ambaye aliingia nafasi ya Correa kipindi cha pili, alikamilisha pasi hiyo kwa ustadi zikisalia dakika tano mechi itamatike.