Kimataifa

Mtu aliyeshambulia waumini kanisani apigwa risasi

February 12th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

JAKARTA, Indonesia

POLISI nchini Indonesia Jumapili walimuua kwa kumpiga risasi mwanamume aliyeshambulia waumini katika kanisa moja akiwa na upanga na kuwajeruhi watu wanne akiwemo kasisi mmoja.

Takriban watu 100 walikuwa wakihudhuria misa katika kanisa moja mjini Sleman, mkoa wa Yogyakarta, wakati mwanamume alipoingia kanisani akiwa na upanga wa urefu wa mita moja na kuanza kuwashambulia watu.

“Watu wanne walijeruhiwa wakati wa kisa hicho- walijeruhiwa vibaya- lakini hatujabaini lengo la mshambuliaji huyo,” msemaji wa polisi wa Yogyakarta, aliambia AFP.

Kulingana na Andhi Cahyo, aliyekuwa kwenye kanisa hilo, kisa hicho kilitokea mtu mmoja alikimbia ndani ya kanisa akitokwa damu kichwani huku mwanamume aliyekuwa na upanga akimfukuza.

“Kila mtu aliogopa na kupiga kemi, nilikuwa niking’ang’ania kumuokoa mke na watoto wangu,” Cahyo aliambia AFP.

Watu waliokuwa kanisani walikimbia nje kupitia mlango mwingine na mshambuliaji akawakimbiza huku akiharibu mali ya kanisa. Mtu huyo alimshambulia kasisi aliyekuwa akisimama kwenye altari.

Polisi walifika baada ya dakika chache. Mtu huyo alielekea alikokuwa afisa mmoja wa polisi akiwa na upanga wake. Afisa huyo alimpiga risasi sehemu ya chini ya tumbo.