Habari

Mtu mmoja auawa Nyeri kwenye mzozo wa ardhi

August 21st, 2019 1 min read

Na NICHOLAS KOMU

@NiqKomu

[email protected]

MTU mmoja amefariki baada ya kuvyogwa kwa panga Jumatano asubuhi kwenye patashika ya kung’ang’ania kipande cha ardhi katika mtaa wa Ngangarithi mjini Nyeri.

Tayari maafisa wa polisi wamewakamata watu 16 ili wakahojiwe kuhusiana na tukio hilo.

Kwa mujibu wa maafisa wa polisi na walioshuhudia, kikundi cha watu 50 kilivamia boma moja viungani mwa mji wa Nyeri wakidhamiria kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye ploti yenye ukubwa wa nusu ekari na ambazo wanadai kumiliki.

Inadaiwa watu hao walitoka Othaya wakiwa wamejihami na wakilenga kutekeleza agizo la mahakama la miaka 10 iliyopita ambalo “lilisema wao ndio wamiliki halali wa kipande hicho cha ardhi.”

Polisi hata hivyo wanaripoti watu hao hawakuwa na notisi ya kuwahamisha waliokuwa wakiishi mahali hapo.

Ubomozi ulikuwa umeanza na ni hapo ndipo wakazi nao walitoka wakiwa wamejihami na kukawa na makabiliano makali; watu wengi wakipata majeraha.

Mwendazake alifariki alipofikishwa katika hospitali ya Rufaa ya Nyeri akiwa na majeraha mabaya kichwani.

“Maafisa wa polisi wamefanikiwa kutuliza hali na pia kuwakamata watu 16 wakahojiwe. Mtu mmoja amefariki mara tu baada ya kufikishwa hospitalini,” amethibitisha kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Nyeri Central Bw Paul Kuria.

Inadaiwa makundi hayo mawili yamekuwa yakizozania mpaka wa vipande viwili vya ardhi kiasi cha kuchukuliana hatua za kisheria kwa mara tano.

Maafisa wa polisi wanachunguza tukio la asubuhi kama mauaji ya kinyama.