Habari Mseto

Mtu na mkewe kizimbani kwa wizi wa shamba la mamilioni

September 14th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKE na mume Alhamisi walishtakiwa kwa kughushi  hatimiliki ya shamba yenye thamani ya Sh20 milioni.

Dkt Joseph Wagura Karanja na Martha Wangui Karanja walifikishwa mbele ya hakimu mkazi mahakama ya Milimani Bi Hellen Onkwani wakikabiliwa na shtaka la kughushi hatimiliki ya shamba na kulimiliki a kwa njia isiyo halali.

Wawili hawa walikana walighushi cheti cha umiliki wa hisa katika shule ya  Busara Forest View Academy Limited ya marehemu Johannes Karanja.

Marehemu na Joseph ni ndugu. Mahakama ilifahamishwa kuwa wawili hao walighushi cheti cha hisa na kuandikisha ardhi ya shule hiyo ya ekari tano yenye thamani ya Sh20milioni inamilikiwa na kampuni ya Busara Computer Point Limited.

“Mheshimiwa mlalamishi katika kesi hii anamiliki asilia mia moja ya kampuni inayomiliki shule hii ya Busara Academy ambayo wakurugenzi wake ni Martha na mume Dkt Karanja mwenye umri wa miaka 70,” wakili anayewatetea aliambia korti.

Hakimu aliombwa awaachilie kwa dhamana. Jambo la kushangaza kampuni ya Busara Computer Point ndiyo inayomiliki shule hii ambayo mwalimu wake mkuu ni Martha.

Korti ilijuzwa Martha amehojiwa kwa muda wa miezi mitatu na mkurugenzi wa jinai (DCI) na kila wakati amekuwa akifika anapohitajika.

“Washtakiwa ni watu wazuri.Mume na Mke. Walifika kortini jinsi waliagizwa na afisi ya DCI. Walikuwa nje kwa dhamana ya Sh100,000.Naomba mahakama iwaachilie kwa kiwango sawa na hicho,” alisema wakili.

Wote waliachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh1 milioni hadi Novemba 4 kesi itakaposikizwa.