Habari za Kitaifa

Mtumiaji WhatsApp aliyemharibia mbunge jina kumlipa Sh2.5m

May 22nd, 2024 2 min read

NA RUTH MBULA

MAHAKAMA moja katika Kaunti ya Nyamira imeamuru mwanachama wa kundi la mtandao wa kijamii, WhatsApp eneo hilo, kumlipa Sh2.5 milioni Mbunge Maalum, Irene Mayaka, kwa kumharibia jina.

Nyaega, almaarufu kama Enchui Ensacha, ambaye pia hupeperusha maudhui kupitia mtandao wa YouTube, alipatikana na hatia ya kutoa matamshi ya kumchafulia sifa mlalamishi kupitia video iliyopeperushwa Julai 25, 2023.

Katika video hiyo iliyoenezwa mno katika makundi kadhaa ya WhatsApp ikiwemo ‘Nyamira News and Updates’ yenye washiriki zaidi ya 457 ambamo Bi Mayaka ni mwanachama vilevile, Nyaega alionekana akijipiga kifua na kujigamba eti mhasiriwa hawezi kumtisha.

Ilibainika pia Nyaega alisambaza video hiyo kwa makundi mengineyo ya WhatsApp ikiwemo ‘The future of Nyamira County’, ‘Nyamaiya & allied forum’ na ‘Egetureri Kiomogusii’ yenye wanachama wasiopungua 400.

Aidha, video hiyo ilipeperushwa kupitia kituo chake cha YouTube kinachofahamika kama ‘Enchui Ensacha TV’, chenye watazamaji waliojisajili zaidi ya 100,000.

Nakala za korti ziliashiria kuwa Nyaega alitumia maneno machafu kuashiria kwamba Bi Mayaka alitumia hila zisizo za kawaida kushawishi uteuzi wake katika Bunge la Kitaifa.

Bi Mayaka aliwasilisha kesi katika Mahakama ya Hakimu mjini Nyamira mnamo Septemba 1, 2023, lakini Nyaega alikosa kufika mahakamani kujitetea licha ya kuitwa.

Hakimu Mkazi, Beniah Okong’o Odhiambo, alibaini kuwa kesi hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa ODM ilikuwa na uzito.

“Korti imekagua kwa kina matini ya taarifa hizo na kutathmini vilevile video pamoja na ushahidi wote uliowasilishwa na mlalamishi na imebaini hakika matamshi hayo yalikuwa ya kuharibu jina na yalinuiwa kuathiri na kutweza hadhi ya mlalamishi katika jamii,” alisema Hakimu.

Hakimu aliamuru Nyaega kumlipa mbunge huyo Sh2 milioni kwa jumla kwa kumchafula jina na kiasi kingine cha Sh500,000 kama “onyo kwa wengine wenye tabia kama hizo na madhara ya kina.”

Aidha, Hakimu alisisitiza kuwa, “sifa ni sehemu ya kimsingi na muhimu kwa hadhi ya mtu binafsi na pindi inapotiwa doa na dai lisilo na mashiko, sifa ya mtu inaweza kuharibiwa milele, hasa ikiwa hakuna fursa ya kutendewa haki.”