Michezo

Mtundu Neymar nje ya kikosi baada ya kujivinjari

February 5th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

SAA 48 tu baada ya kusherehekea siku ya kuzaliwa kwake kwenye mkahawa mmoja wa kifahari jijini Paris, staa Neymar aliondolewa ghafla katika kikosi cha Paris Saint-Germain (PSG) kilichotarajiwa kucheza na Nantes Jumanne usiku, kutokana na jeraha la ubavuni.

Raia huyo wa Brazil alicheza mechi nzima Jumamosi ambayo klabu yake ilinyuka Montpellier 5-0.

Hata hivyo, kulikuwa na madai kwamba Neymar pamoja na wenzake wa PSG walikuwa wamelemewa na maruerue baada ya kukesha usiku kucha katika mkahawa wa Yoyo karibu na jumba la Eiffel Tower.

Lakini alipoulizwa kusema lolote kuhusu dai hilo, kocha Thomas Tuchel alikwepa akisema jukumu lake ni kuunda kikosi shupavu cha kukabiliana vilivyo na Nantes, katika pambano hilo la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

“Kawaida kunapokuwa na sherehe kama hii, ni vigumu kuwazuia wachezaji kuhudhuria. Lakini kikosi cha kucheza kipo. Sitakubali watu waanze kushambulia wachezaji wangu kuhusiana na madai haya. Mie sitaweza kumuadhibu mchezaji yeyote kutokana na hilo.”

Kylian Mbappe alitarajiwa kujaza nafasi ya Neymar, siku chache baada ya kufokeana na kocha wake alipoondolewa uwanjani na nafasi yake kupewa Mauro Icardi.

Kuhusu kisa hicho kilichotokea ugani Parc des Princes, kocha Tuchel alisema ni kawaida kwamba wachezaji hawapendi kutolewa kwa mechi.

“Sina uhasama wowote na Mbappe, lakini nitaendelea kuwapa nafasi wale wanataka kucheza kwa kujitolea. Mvutano ulikuwa kati ya mchezaji ambaye hakutaka kutolewa, na kocha ambaye alitaka kufanya kazi yake kwa kuhakikisha amewapa nafasi walio tayari kutumikia timu kikamilifu.”

Mbappe mwenye umri wa miaka 21 alikuwa amefunga bao katika ushindi huo mnono, kabla ya kurushiana maneno ya Tuchel.

Kocha alisema alijadili tukio hilo na mkurugenzi wa klabu, Leonarndo siku hiyo hiyo.

“Nilizungmza naye Jumapili kwa sababu kuna wachezaji wengi wenye tabia kama hiyo, ambao awali wamekosa kuniheshimu. Lakini niliyoyasema yatabakia kuwa siri,” aliongeza kabla ya mechi ya jana usiku.

“Kwangu, nilifanya uamuzi uliofaa kwa vile tulikuwa tukiongoza kwa idadi nzuri ya mabao. Nikaonelea nimtoe Pablo na Kylian ili kuwaingiza Mauro na Edison Cavani. Naelewa ni vigumu kwa wachezaji fulani, lakini ni kawaida michezoni kushuhudia hali kama hii.”