Makala

Mtunze mbwa akufae zaidi

May 9th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

RATIBA ya kila siku ya Bw Nicholas Ng’ang’a, mfugaji wa mbwa Kiambu, huwa yenye shughuli tele.

Araukapo alfajiri na mapema, hatua ya kwanza huwa kufanya usafi katika makazi ya wanyama hawa ambao ni waaminifu zaidi.

“Ukimtunza mbwa, atakutunza kwa kuwa ni mwaminifu. Usafi kwake ni muhimu; kuanzia mazingira anamoishi, chakula, na maji,” anasema Bw Nicholas.

Baada ya usafi wa hadhi ya juu, huwatilia mlo wakati huohuo akikagua hali yao kuona iwapo kuna aliye na udhaifu wowote ule.

Kijana huyu anafuga mbwa wa kunusa, wa ulinzi na wa kuongoza, na vilevile wa kurembesha mazingira, kutokana na umaridadi wao wa rangi.

Aina ya mbwa

Nicholas hufuga mbwa aina ya German shepherdBore BellsGolden Retriever na Rot Wailers. Pia, ana Labrador, RetrieverMaltese na Terrier.

Alianza ufugaji wa wanyama hawa 2009, kwa mtaji wa Sh20, 000 pekee, pesa alizoweka akiba tangu akiwa shule ya upili. Alinunua mbwa wa kike aina ya Golden Retriever kwa mtaji huo, akakodi wa kiume ili kumtunga ujauzito.

Mapenzi yake kwa mbwa yalijiri tangu akiwa mdogo, akieleza kwamba utotoni alilelewa nao.

“Baba alikuwa na mbwa niliyempenda kwa dhati, alikuwa akinisindikiza shuleni asubuhi na nitokapo majira ya jioni la kushangaza ningempata nje ya lango la shule,” asimulia mfugaji huyu.

Mwaka wa 2010 licha ya kushinikizwa na wazazi wake asomee kozi ya umekanika, Bw Nicholas anadokeza kwamba aliisomea kwa muda wa miezi mitatu pekee halafu akaiacha. Hii ni kutokana na mapenzi ya dhati aliyo nayo kwa wanyama, akakata kauli ya kuwafuga na kuikumbatia kama ajira.

Bei

Ni shughuli inayomuingizua donge nono, kwani mbwa mmoja aliyekomaa humuuza zaidi ya Sh100, 000. Kilebu, kikembe wa mbwa, mmoja hapungui Sh35, 000.

Nicholas 28, anasema ufugaji wa mbwa ni shughuli rahisi mno kuendesha. Waliokomaa hulishwa mara moja kwa siku, ilhali vilebu hula mara mbili kwa siku. Chakula cha mbwa ni nyama, mifupa iliyosagwa, samaki aina ya ‘omena’, na masalia ya mlo wa binadamu. Pia, kuna chakula maalum cha mbwa kinachojulikana kama ‘top dog’.

Wataalamu wa masuala ya ufugaji wanahimiza mbwa kulishwa chakula chenye madini kamilifu. “Kinapaswa kuwa na Protini, Wanga na Vitamini. Ni wanyama kama wengine, wanahitaji maji safi na kwa wingi,” aeleza Bw Simon Wagura, mtaalamu wa kilimo na ufugaji.

“Ili kuongeza Vitamini mbali na chakula chenye madini haya, hutiliwa CAL-VITAMAX, ambayo pia ina Calcium ndani yake,” anasema mdau huyu, ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya Country Farm, inayohusika na masuala ya kilimo na ufugaji.

Ili kudhibiti vimelea kama viroboto na kupe katika makazi ya mbwa, Bw Wagura anahimiza kupulizia dawa kama vile Dudu Dust. Huwaosha kwa maji yaliyochanganywa na dawa aina ya Dudu Krin, ili kuua vimelea.

Mazoezi kwa njia ya kutembezwa

Kulingana na Nicholas Ng’ang’a yote hayo yanaweza kuwa bure bilashi ikiwa mbwa hawatapata muda wa kuvuta hewa mwanana nje ya mazingira yao kwa kutembezwa.

“Wanapaswa kufanya mazoezi kwa njia ya kutembezwa nje ya wanakoishi ili kuwanyoosha viungo vya mwili,” anafafanua mfugaji huyu.

Ni muhimu kutaja kuwa miale ya jua huifanya mifupa ya binadamu na wanyama kuwa imara, dhabiti na yenye nguvu. Pia, inasemekana huchangia Vitamini D katika mwili.

Nicholas hufanya shughuli ya kuwatembeza majira ya jioni kila siku. Ni hatua ambayo huitekeleza kwa usaidizi wa mfanyakazi wake, aliyemuajiri kwa madhumuni ya kumsaidia kuendesha ari yake ya ufugaji wa mbwa.

Huwatembeza wakiwa wamefungwa kwa nyororo shingoni kwani ni hatari kwa usalama wa wapitanjia.

Pia, hutumia fursa hiyo kuwafunza kutangamana na watu na vilevile kunusa.

“Ni shughuli muhimu kwa sababu hujua umachachari wa kila mbwa na kujua ninapopaswa kupevusha na kuwakosoa,” anaelezea.