Mturuki mwandani wa Dkt Ruto afurushwa nchini

Mturuki mwandani wa Dkt Ruto afurushwa nchini

Na CHARLES WASONGA

MFANYABIASHARA Harun Aydin ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto, Jumatatu alfajiri alisafirishwa kwa nguvu hadi nchini mwake Uturuki, siku ambayo alitarajiwa kuwasilishwa mahakamani kufunguliwa mashtaka ya ugaidi.

Kulingana na wakili wake Ahmednassir Abdullahi, serikali ya Kenya ilichukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwa haikuwa na ushahidi wa kuhimili kesi dhidi ya Aydin.

“Nimethibitisha kuwa Harun Aydin alirejeshwa nchini mwake saa kumi alfajiri. Serikali iligundua kuwa haingeweza kuhimili kesi ya uhalifu dhidi yake,” Bw Abdullahi, almaarfu, Grand Mullar, alisema kupitia akaunti yake ya Twitter.

Wakili huyo mkuu – SC – alisema alikuwa tayari kumwakilisha raia huyo wa Uturuki katika mahakama ya kusikiliza kesi za ugaidi iliyo eneo la Kahawa West, Kaunti ya Kiambu.

Bw Abdullahi pia aliapa kuwasilisha kesi mahakamani kutaka kwamba Bw Aydin arejeshwe nchini ili afunguliwe mashtaka kwa mujibu wa sheria.

“Unawezaje kumkamata mtu barabarani kwa madai kuwa anafadhili ugaidi kisha kama serikali unakosa ujasiri wa kumleta mahakamani ili kufanikisha kushtakiwa kwake? Hii inaonyesha kuwa serikali hii ni dhalimu na haina haya,” akawaambia wanahabari nje ya mahakamani hiyo.

Akaongeza: “Kama mawakili wake tutapinga hatua ya kumfurusha nchini kwa sababu iliendeshwa kinyume cha sheria na taratibu zilizowekwa. Serikali haiwezi kumfurusha mtu kwa sababu ni rafiki ya Naibu Rais. Hiyo sio hatia. Kwa hivyo, tutapinga hatua hiyo na kumrejesha Aydin nchini mwaka huu au mwaka ujao au mwaka mwingine.”

Bw Aydin alikamatwa Jumamosi katika uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi muda mfupi baada ya kuwasili nchini kutoka Uganda.

Mgeni huyo ambaye Dkt Ruto amedai kuwa ni mwekezaji halali, alikuwa miongoni mwa wandani wa naibu huyo wa rais walioratibiwa kuandamana naye Uganda kwa kile kilichotajwa kama ziara ya kibinafsi.

Hata hivyo, Dkt Ruto alizuiwa kusafiri lakini wandani wake, wakiwemo wabunge Oscar Sudi (Kapseret), Ndindi Nyoro (Kiharu) na Benjamin Tayari (Kinango) waliruhusiwa kusafiri hadi Uganda.

You can share this post!

Shevchenko aacha kazi ya ukocha katika timu ya taifa ya...

Real Madrid na AC Milan nguvu sawa huku Bale akipoteza...