Makala

MUAFAKA: Kamati ya pamoja kuzuru kaunti zote 47 kupata maoni ya Wakenya

November 7th, 2018 3 min read

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya Kitaifa la Maridhiano (Building Bridges Initiative) imeanza vikao vyake vya kufanya mashauriano na kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali katika nyanja za dini, biashara, siasa na vijana.

Mmoja wa makatibu wa kamati hiyo Paul Mwangi (pichani juu) alisema vikao hivyo vitakavyofanyika katika ukumbi wa Jumba la Mikutano ya Kimataifa ya Kenyatta (KICC) ni vya kwanza kati ya msururu wa mikutano ambayo yataendeshwa kote nchini kuanzi mwishoni mwa juma lijalo.

Kwenye mahojiano na wanahabari Bw Mwangi alisema kamati hiyo ya wanachama 14 itazuru miji mbalimbali katika kaunti zote 47 kukusanya maoni kutoka kwa umma.

“Tutakusanya maoni kuhusiana na masuala tisa ambayo yaliratibiwa katika muafaka wa maelewano ambayo Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga walitia saini mnamo Machi 9. Masuala hayo ni kama ufisadi, ugatuzi, maadili ya kitaifa, ujumuishaji kati ya mengi,” akasema.

Naibu mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano Adams Oloo ahutubia wanahabari. Picha/ Charles Wasonga

Bw Mwangi, alisema shughuli za Kamati hiyo hazitaathirika na mjadala wa sasa kuhusu mabadiliko ya katiba kwa njia ya kura ya maamuzi, akisema suala hilo haliko katika ajenda yao.

“Suala la kura ya maamuzi haliko katika orodha ya masuala ambayo kamati yatashughulikia. Lakini wananchi wako huru kulizungumzia watakapokuwa wakitoa maoni yao kuhusu dawa mjarabu wa shida ya fujo za kisiasa na migawanyiko ambayo hushuhudiwa nchini kila baada ya uchaguzi,” akasema wakili Mwangi, kauli ambayo iliungwa mkono na mwenyekiti wa kamati hiyo Seneta Yusuf Haji.

Baada ya wiki moja ijayo kamati hiyo itazuru kaunti za Makueni, Kitui na Machakos katika awamu ya pili ya kukusanya maoni kutoka kwa umma.

Naye Naibu mwenyekiti Dkt Adams Oloo alisema kamati hiyo itatoa mwelekeo wake kuhusu suala hilo la mageuzi ya katiba baada ya kusikiza maoni na mapendekezo kutoka kwa wananchi.

“Tunaweza kukubaliana na kile ambacho wanasiasa wanasema au kutofautian nao. Lakini kwa wakati huu suala hilo sio mojawapo ya masuala tunayoyashughulikia,” akasema Dkt Oloo ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Askofu Ben Njoroge wa muungano wa makanisa ya kievanjelisti Kenya (EAK). Picha/ Charles Wasonga

Bw Haji ambaye ni Seneta wa Garissa alisema ni wakati wa kuandaa ripoti ambapo tubaini ikiwa umma wanaunga mkono suala hilo au la.

Mnamo Alhamisi kamati hiyo ilipokea maoni na mapendekezo kutoka kwa makundi ya wadau kama vile Baraza la Waislamu Nchini (Supkem), Muungano wa Makanisa ya Kievanjelisti Nchini (EAK), Baraza la Wahindu Nchini (HCK).

Baraza hilo pia lilipokea maoni kutoka kwa Kituo cha Demokrasia ya Vyama Vingi (CMD), Muungano wa Sekta ya Kibinafsi (KEPSA), Chama cha Wafanyabishara na Viwanda (KNCCI) na Muungano wa Vyama vya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu.

Wanakamati wakiwa kwa kikao. Picha/ Charles Wasonga

Katika mawasilisho yake, Naibu Mwenyekiti wa Supkem Hassan Ole Naado ilipendekeza suala ya makundi yaliyotengwa liangaliwe kwa makini akisema kuna makundi mengi ambayo yamechipuza yakihadaa kuwa yametengwa.

“Kamati hiyo inapasa kutusaidia kuchambua na suala la makundi ya waliotengwa ikizingatiwa kuwa pesa hutengwa kwa ajili ya kuinua maeneo na makabila yaliyoachwa nyuma kimaendeleo.

Baraza hilo pia lilipendekeza kuwa wananchi wahamasishwe kikamilifu katika vita dhidi ya makundi ya wahalifu sugu kama vile Alshabaab.

“Makundi kama hayoa ya Al Shabaab yamekuwa yakileta migawanyiko ya kidini nchini. Kwa hivyo, dawa mjarabu wa kutatua changomoto hii ni kupitia kushirikishwa kwa wananchi katika vita vya kuangamiza makundi kama hayo,” akasema Ole Naado.

Connie Kivuti, Katibu Mkuu wa EAK. Picha/ Charles Wasonga

Naye Katibu Mkuu wa EAK Bi Connie Kivuti alisema alipendekeza kuwa idadi wabunge na madiwani ipunguzwe sawa na idadi ya kaunti.

“Tungependekeza kuwa idadi ya maeneo bunge isalie kama zamani yaani 210 na nyadhifa za wabunge maalum ziondolewe. Kaunti pia zipunguzwe kutoka 47 hadi 15” akasema.

Hata hivyo, hakupendekeza jinsi shughuli ya kupunguzwa kwa maeneo hayo ya uwakilishi itafanywa.

Naye mwenyekiti wa CMD Bw Omingo Magara aliitaka kamati hiyo kupendekeza kuwa vyama vidogo vya kisiasa vipewe ufadhili ili viweze kuendesha shughuli zao ipasavyo.

Vile vile, aliwataka Wakenya kubadili mielekeo yao kuhusu tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kuwa kujenga imani yao kwake.

“Shida kuu inayoathiri mfumo wa uchaguzi nchini ni kuwa wanasiasa na Wakenya kwa jumla wamekosa imani ya IEBC kutokana na sababu za kisiasa na kikabila. Tunapaswa kuiga mfano wa Denmark ambapo washiriki na wananchi wana imani kwa mfumo wa uchaguzi,” akasema Bw Magara ambaye zamani alikuwa Mbunge wa Mugirango Kusini.

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia ya Vyama Vingi nchini Bw Omingo Magara. Picha/ Charles Wasonga

Mwenyekiti huyo wa CMD pia alisema kuwa IEBC inapasa kugatuliwa hadi katika maeneo ya mashinani ili kuondoa changamoto kadhaa inayokabili tume hiyo wakati huu.

“Tuwe na tume huria katika maeneo ya wadi na maeneo bunge ambazo zitaendesha chaguzi kule. Hatua hii itatoa nafasi kw tume ya kitaifa kuandaa na kuendesha chaguzi za urais pekee,” akapendekeza Bw Magara.

Kamati hiyo ya maridhiano imepewa muda wa kuaandaa na kuwasilisha mapendekezo yao kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga. Ripoti hiyo inapasa kusheheni mbinu za kukabiliana na ukabila, ufisadi, siasa za migawanyiko, na changamoto zingine ambazo huleta migawanyiko.

Kamati hiyo ilibuniwa baada ya Machi 9 wakati Rais Kenyatta na Bw Odinga walipotia muafaka wa maelewano na kuzika tofauti zao za kisiasa, zilizoleta maafa na machafuko baada ya uchaguzi mkuu uliopita.

Imepewa ufadhili wa kima cha Sh100 milioni ili iweze kuendesha shughuli zake.