Michezo

Muchiri wa Tusker mwenye kiatu cha dhahabu KPL ang'aa

August 22nd, 2018 1 min read

NA CECIL ODONGO

WINGA wa Tusker FC Boniface Muchiri anaendelea kung’aa katika ligi ya KPL msimu huu baada ya kufuma wavuni mabao manane na kuchangia mara saba mabao mengine yaliyofungwa na wenzake timuni.

Muchiri ambaye alifunga bao la ushindi wakati mabingwa hao mara 11 wa KPL waliposhuka dimbani Jumapili Agosti 19 kuvaana na Zoo Kericho FC, sasa anasema atazidi kuyanoa makali yake akilenga kuzidi kutingisha nyavu za wapinzani.

“Nimefurahi sana kwamba nililifunga bao la ushindi. Kwa sasa nafurahia uwepo wangu kambini mwa Tusker na nashukuru kila mtu kwa sapoti yao iliyochangia fomu nzuri ninayojivunia,” akasema Muchiri.

Aidha ameongeza kwamba lengo lake kuu ni kutumia kuimarika kwake kuzidi kuyafunga mabao ili kuimarisha nafasi ya Tusker katika msimamo wa jedwali la KPL.

“Nimeimarika sana tangu nijiunge na klabu hii na nimekuwa huru kusakata boli uwanjani. Talanta pekee haitoshi, lazima ujibidishe kila siku ili utambe na upate fomu ya kutisha,” akadai Muchiri.

Mabingwa hao wa mwaka wa 2016 wapo katika nafasi ya tano kwa alama 39 baada ya kujibwaga uwanjani mara 27 na Agosti 25 watakuwa wageni wa mabingwa wa mwaka 2006 SoNy Sugar katika uga wa Awendo Green Stadium.