Habari

Muda wa marufuku ya ada ya nyumba waongezwa

May 20th, 2019 1 min read

Na SAM KIPLAGAT

SERIKALI Jumatatu ilipata pigo baada ya Mahakama ya Leba kuongeza muda wa marufuku inayoizuia kukata asilimia 1.5 ya mishahara ya wafanyakazi kugharimia mradi wa ujenzi wa nyumba hadi Mei 27.

Jaji Maureen Onyango alisema miungano kadhaa ya wafanyakazi imewasilisha kesi kupinga utekelezaji wa mradi huo. Aliagiza wahusika wote kufika kortini Mei 27 ili kesi hizo zijumuishwe kabla ya mwelekeo zaidi kutolewa.

Miungano iliyowasilisha pingamizi zao kuhusu mradi huo ni Muungano wa Waajiri Kenya (FKE), Muungano wa Watumiaji Bidhaa (COFEK), Muungano wa Wafanyabiashara (TUC), Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi (KNUN) huku Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU) ukiwa ndio uliwasilisha kesi ya kwanza kortini.

FKE iliwasilisha kesi katika mahakama ya Milimani dhidi ya Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) kwa kuagiza waajiri kuwasilisha fedha za waajiriwa kuanzia mwezi huu wa Mei bila kuzingatia kwamba kesi kuhusu makato hayo bado ipo kortini.

KRA hata hivyo ilijitetea kwa kudai haikutajwa popote kwenye kesi iliyowasilishwa na miungano hiyo dhidi ya serikali, na inafaa kuruhusiwa kukusanya mapato hayo kwa kuwa mswaada wa fedha 2018 ulijumuisha maoni ya umma kabla ya kupitishwa bungeni.

Wakili wa Cofek, Henry Kurauka alisema ushuru huo unakinzana na sheria ya uajiri na notisi kuhusu kutekelezwa kwake ilitolewa haraka wala maoni ya wafanyakazi hayakuzingatiwa.

“Watakaochangia fedha zao kupitia makato hayo ya kila mwezi hawajahakikishiwa kwamba watapata nyumba baada ya kuwekeza fedha zao,” akasema Bw Kurauka.

Hata hivyo, COTU kupitia wakili wake Okwe Ochiando alieleza mahakama kwamba wamewasilisha ombi la kuondoa kesi waliyowasilisha baada ya serikali kushughulikia malalamishi waliyoyaibua.

Serikali mwezi Aprili ilitoa notisi ya kuipa KRA mamlaka ya kukusanya fedha za mradi huo pamoja na makato mengine. Wakenya ambao hawana ajira wanaweza kuchangia mradi huo kwa kutoa Sh200 kila mwezi japo kwa hiari yao.