Michezo

Muda wa Pogba kambini mwa Man-United umekwisha na ataondoka mwishoni mwa msimu huu – ajenti

December 8th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

PAUL Pogba “hafurahii maisha” kambini mwa Manchester United na itamlazimu “kutafuta kikosi kipya” katika muhula ujao wa uhamisho wa wachezaji.

Mkataba wa sasa kati ya Pogba na Man-United unatarajiwa kutamatika rasmi mnamo Juni 2022.

Haya ni kwa mujibu wa wakala wake, Mino Raiola.

Pogba, 27, amechezeshwa mara nane pekee katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ambapo amepangwa katika kikosi cha kwanza cha waajiri wake mara tano. Bao lake la kwanza katika kampeni za msimu huu ni lile alilofunga dhidi ya West Ham United katika ushindi wa 3-1 uwanjani London Stadium mnamo Disemba 5, 2020.

“Pogba hana raha. Hawezi tena kujieleza jinsi anavyotaka na kwa namna anavyotarajiwa afanye,” akasema Raiola katika mahojiano yake na gazeti la Tuttosport nchini Italia.

“Itamlazimu abadilishe timu. Inabidi abadilishe hewa. Ipo haja aondoke Man-United kwa sababu hajivunii kuwa katika zizi la Old Trafford,” akasema Raiola.

“Ana mkataba ambao utakamilika baada ya mwaka mmoja na nusu. Lakini nahisi kwamba suluhu bora ni kwa sogora huyo kuagana na Man-United ambao nadhani watakuwa radhi kumtia mnadani mwishoni mwa kampeni za msimu wa 2020-21,” akaongeza ajenti huyo kwa kusisitiza kwamba mteja wake hana nia yoyote ya kurefusha muda wa kuhudumu kwake uwanjani Old Trafford kwa kutia saini kandarasi mpya na Man-United.

Pogba ambaye alijiunga mpya na Man-United kutoka Juventus ya Italia kwa kima cha Sh12 bilioni mnamo 2016, amewahi kufichua maazimio ya kujiunga na Real Madrid ya Uhispania.

Mnamo Novemba 2020, kocha Didier Deschamps wa timu ya taifa ya Ufaransa alisema kwamba Pogba “hawezi kufurahia” hali yake ya sasa kambini mwa Man-United kwa kuwa “anapuuzwa na kutothaminiwa”.

Katika kampeni za msimu uliopita wa 2020-21, Pogba aliwajibishwa mara 22 pekee katika mashindano yote baada ya kupata jeraha baya la kifundo cha mguu.

Ingawa hivyo, Raiola alifichua mnamo Agosti kuhusu uwezekano wa Pogba kupokezwa kandarasi mpya uwanjani Old Trafford na akasisitiza kwamba alitarajia mazungumzo kuhusiana na suala hilo kuanza mwishoni mwa Januari 2021.

“Muda wa Pogba ugani Old Trafford umekwisha. Hakuna haja ya kuzungukia kando kando. Ni vyema kusema ukweli na inavyosatahili. Huu ni wakati wa kutazama mbele na kuacha kupoteza wakati kambini mwa Man-United,” akasema Raiola.