Mudavadi afichua sababu ya kugura OKA

Mudavadi afichua sababu ya kugura OKA

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amesema aliondoka kutoka muungano wa One Kenya Alliance (OKA) baada ya kusalitiwa na vinara wenzake, Kalonzo Musyoka na Gideon Moi.

Akiongea Jumapili, Januari 30, 2022, baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika Kanisa la St Faith, Rongai, Kajiado, Bw Mudavadi alidai kuwa alipata habari kuwa wawili hao wamekuwa wakifanya mikutano ya kisiri na kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga.

“Niliamua kufuata mkondo mwingine baada ya kugundua kuwa Moi na Kalonzo walikuwa wameegemea mrengo wa Azimio la Umoja unaongozwa na Raila. Hii ilionyesha wazi kwamba nyoyo zao hazikuwa kwa OKA bali kwa Raila Odinga. Wenzangu walikuwa wanaegemea mradi wa serikali ambao ni Raila Odinga; mwanasiasa ambaye amezoea siasa za kuwatumia wenzake kwa manufaa yake kisha kuwatelekeza.” Bw Mudavadi akawaambia wanahabari baada ya ibada.

Kiongozi huyo wa ANC alisema kwa kufuata mkondo wa kuungana na chama cha United Democratic Alliance (UDA) hakusaliti mtu yeyote, bali alitaka kuendeleza mkondo ambao unaungwa na Wakenya wengi.

Bw Mudavadi alisema wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa ANC (NDC) katika Bomas of Kenya, alionywa dhidi ya kuunga mkono Azimio la Umoja na kiongozi wake, Bw Odinga.

“Katika NDC, wajumbe wa ANC waliniamba wazi kwamba nisiungane na Azimio ambao ni mradi wa serikali na Wakenya hawataki,” akasema.

Mbw Musyoka na Moi waliondoka katika mkutano huo wa ANC walipopata habari kwa Naibu Rais William Ruto na wafuasi wake walitarajiwa kuhudhuria.

Waliandamana na mfanyabiashara na mgombeaji urais Jimmi Wanjigi pamoja na Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo, ambaye ni mwanachama wa ANC.

You can share this post!

MWALIMU WA WIKI: Mwandishi stadi na mlezi wa vipaji

Kakamega yanasa 3, yataka moja ikafunge

T L