Na WANDERI KAMAU
KIONGOZI wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi, Alhamisi aliwafokea vikali vigogo wengine wa kisiasa wanaowania urais, akisema wameanza kumwiga kuhusu mikakati ya kufufua uchumi wa nchi.
Bw Mudavadi alisema kuwa yeye ndiye aliyeanza mdahalo kuhusu haja ya kutaka kufufua uchumi na kubuni nafasi za ajira nchini, baada ya kubaini mwelekeo wa kiuchumi wa nchi haukuwa wa kuridhisha.
“Nilibaini kuhusu mwelekeo mbaya wa kiuchumi wa nchi mnamo 2018, wakati wabunge walipitisha Mswada wa Fedha kuiruhusu serikali kuongeza ushuru wa bidhaa mbalimbali za kimsingi,” akasema Bw Mudavadi, akisema huo ndio ulikuwa mwanzo wa masaibu yanayowakumba Wakenya, kama vile gharama ya juu ya bei za mafuta.
Alisema vigogo hao “wanadandia” kuhusu sera zake, akieleza ni wakati wawaeleze Wakenya bayana kuhusu mikakati watakayoweka kuboresha maisha yao ikiwa watachaguliwa kama rais 2022.
Bw Mudavadi alionekana kumlenga Naibu Rais William Ruto, ikizingatiwa amekuwa akishikilia ndiye aliyeanzisha mdahalo kuhusu haja ya kufufua uchumi.
Dkt Ruto amekuwa akiendeleza kampeni yake kwa kauli ya kufufua uchumi kuanzia kiwango cha chini, maarufu kama “Bottom up”, akishikilia ndiyo njia ya pekee kuhakikisha Wakenya wa kiwango cha chini wanachangia kwenye harakati za kuinua uchumi.
Kiongozi wa ODM, Raila Odinga pia ameanza kuelekeza kampeni zake za kuwania urais kwenye juhudi za kuinua tena uchumi.
Bw Odinga amekuwa akitoa taarifa kuhusu hatua atakazochukua kufufua sekta muhimu kama kilimo na kubuni ajira, hasa miongoni mwa vijana, wanawake na watu walemavu.
“Ni vizuri wakati sote tunapoangazia mikakati ya kuboresha uchumi, ijapokuwa ni sisi (ANC) tuligundua tatizo hilo na kutangaza juhudi za kuufufua tena,” akasema.
Bw Mudavadi amekuwa akiilaumu serikali ya Jubilee kwa kuharibu ukuaji wa uchumi wa nchi, akikosoa utaratibu wake katika kuchukua mikopo kutoka nchi za nje, hasa China.
Kufikia sasa, Kenya inakisiwa kuwa na deni la zaidi ya Sh8 trilioni.Katika kujitetea kwake, serikali imekuwa ikisema kiwango kikubwa cha madeni hayo kimekuwa kikitumika kufadhili ujenzi wa miundomsingi muhimu kama barabara, reli na kusambaza umeme miongoni mwa Wakenya.
Majuzi, Shirika la Fedha Duniani (IMF) liliiorodhesha Kenya kwenye orodha ya nchi ambazo kiwango chake cha deni “si cha kuridhisha.”
Bw Mudavadi alitoa kauli hiyo Alhamisi kwenye hafla maalum jijini Nairobi, ambapo chama hicho kilitangaza uteuzi wa Bw Simon Kamau kama Katibu Mkuu Mpya.
Uteuzi huo unafuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Barrack Muluka, aliyejiunga na kambi ya Dkt Ruto kama mshauri wa mikakati ya kisiasa ielekeapo 2022.
Ikizingatiwa Bw Kamau anatoka katika Kaunti ya Murang’a, juhudi hizo zinaonekana kama hatua ya vigogo wa kisiasa kuendelea kutafuta uungwaji mkono wa kisiasa katika eneo hilo, ambalo ni ngome ya kisiasa ya Rais Kenyatta.
Majuma kadhaa yaliyopita, Bw Mudavadi alisema huenda akamteua mgombea-mwenza kutoka ukanda huo.
Dkt Ruto, Bw Odinga na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, pia wamekuwa wakifanya ziara mbalimbali katika eneo hilo, wakiahidi kulijumuisha kwenye serikali zao ikiwa wataibuka washindi kwenye uchaguzi ujao.