Mudavadi akoroga hesabu katika UDA

Mudavadi akoroga hesabu katika UDA

MWANGI MUIRURI NA LEONARD ONYANGO

HATUA ya Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi kuungana na Naibu wa Rais William Ruto imevuruga hesabu za baadhi ya wanasiasa wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Hii ni baada ya Bw Mudavadi na Kinara wa Ford Kenya Moses Wetang’ula kuibuka kuwa wenye ushawishi mkubwa ndani ya muungano wa Kenya Kwanza, ikilinganishwa na viongozi wa UDA waliokuwa karibu na Dkt Ruto awali kama vile mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua na mwenzake wa Garissa Mjini, Aden Duale.

Hofu pia imetanda miongoni mwa viongozi wa UDA hasa kutoka eneo la Mlima Kenya kwamba huenda Dkt Ruto akateua Bw Mudavadi kuwa mwaniaji mwenza wake.

Mnamo Desemba 2021, Dkt Ruto alipokuwa katika Kaunti ya Nyeri, alidokeza kuwa huenda akamteua Bw Gachagua kuwa mwaniaji wake.

“Nawaombeni wakazi wa Mathira, mruhusu Gachagua aandamane na mimi katika maeneo mengine ya nchi ili tushinde hiki kiti cha urais. Mniachie ili tuendeshe naye siasa za kitaifa,” alisema Dkt Ruto.

Lakini baadhi ya wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya waliozungumza na Taifa Leo walionyesha hofu kuwa huenda Naibu wa Rais akabadili nia baada ya Bw Mudavadi kujiunga na kambi yake.

Lakini Seneta wa Murang’a Bw Irungu Kang’ata ameshikilia kuwa kiti cha mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto bado ni cha wakazi wa Mlima Kenya.

“Wao wamekuja kutafuta ushirika. Sisi nasi tulikuwa ndani ya UDA wakija. Kuna yale maafikiano ambayo tuko nayo tayari katika safari hii ya kujenga na kuthibiti mrengo wa ‘Hasla’. Hakuna mambo ambayo yameharibika na tuko shwari kama Mlima Kenya,” akasema.

Mgombea mwenza

Bw Kang’ata alisema kwamba Kaunti ya Murang’a tayari imependekeza majina ya watu wawili kuwa mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto.

“Tumetoa majina ya mbunge wa Kandara, Alice Wahome na mwenzake wa Kiharu, Ndindi Nyoro. Hatuna shaka kwamba wadhifa huo utamwendea mtu wa Mlima Kenya,” akasema.

Mwanasiasa wa UDA anayewania useneta wa Murang’a kupitia UDA, Joe Nyutu anasema wanasiasa wa Mlima Kenya ndio walimsukuma Dkt Ruto akawasake Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula ili ajiongezee kura.

Ushirikiano baina ya Dkt Ruto na Bw Mudavadi pia unatishia kuzima ndoto ya baadhi ya wanasiasa wa UDA ambao wamekuwa wakimezea mate viti mbalimbali.

Jumanne, Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja na mbunge wa zamani wa Starehe, Margaret Wanjiru nusura wazabane makonde mbele ya Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula muungano wa Kenya Kwanza ulipokuwa ukijipigia debe katika eneo la City Park mtaani Parklands, Nairobi.

Wawili hao wanataka kiti cha ugavana wa Nairobi.Bi Wanjiru anaungwa mkono na Naibu wa Rais Ruto huku Bw Sakaja akiungwa mkono na Bw Mudavadi.

Katika Kaunti ya Kakamega, hesabu ya seneta wa zamani Boni Khalwale kuwa gavana inaonekana kuvurugika baada ya seneta wa sasa wa kaunti hiyo Cleophas Malala wa ANC kujitosa ulingoni.

Kabla ya Bw Mudavadi kujiunga na Dkt Ruto, Dkt Khalwale alionekana kuwa kifua mbele kunasa tiketi ya UDA, lakini sasa hesabu zake zinaonekana kuvurugika.

Hali hiyo pia imetoa mwanya kwa wanasiasa wa mrengo wa Azimio la Umoja unaoongozwa na Raila Odinga kujaribu kushawishi wakazi hasa wa Mlima Kenya kuwa Dkt Ruto hatateua mtu kutoka eneo hilo kuwa naibu wake kama ambavyo amekuwa akiahidi.

Wanasiasa hao wakiongozwa na Waziri wa Kilimo, Peter Munya na mbunge wa zamani wa Gatanga, Peter Kenneth wanaendesha kampeni kuwa Naibu Rais amekuwa akiwahadaa kwamba atawapa wadhifa wa naibu wa rais, lakini sasa atakabidhi wadhifa huo kwa Bw Mudavadi.

Dkt Ruto hajasema lolote kuhusu madai hayo.

You can share this post!

‘Jungle’ ajitenga na harakati za chama cha UDA

TAHARIRI: Wadau waepushe raia kususia kura katika uchaguzi...

T L