Habari

Mudavadi alitaka jopo la BBI kuhakikishia Wakenya ripoti hailengi kubuni nafasi za uongozi kwa watu kadhaa

February 18th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC)Musalia Mudavadi amefike mbele ya jopo la mpango nwa maridhiano (BBI) ambapo ametoa maoni yake.

Akizungumza Jumanne katika jumba la mikutano la KICC, Mudavadi amelitaka jopo kuwahakikishia Wakenya kwamba ripoti hiyo hailengi kuwahalalishia baadhi ya viongozi nafasi bila kujali mahitaji ya raia.

“Ipo haja ya jopo hili kuwahakikishia Wakenya kwamba ripoti hii hailengi kubuni nafasi za uongozi kwa watu kadhaa,” amesema Mudavadi.

Ametaka ripoti hiyo itekelezwe itakapokuwa tayari ili kuepukana na matukio ya awali ambapo ripoti ziliandaliwa na tume zilizotumia raslimali za mlipa ushuru lakini baadaye zikawekwa kando.

“Tunaomba kwamba ripoti ya BBI haitawekwa kando na kutotekelezwa kama ripoti za hapo awali kama ripoti za Waki, Kiliku, Ndung’u, TJRC kati ya nyinginezo,” amesema.

Amependekeza kubuniwa kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Deni la Taifa (PDMA) katika kiwango cha kitaifa na serikali za kaunti.

Mamlaka hii itakuwa na jukumu la kuishauri serikali na kuweka wazi maelezo yote kuhusu deni la taifa kwa umma.

Amesema ANC inaandaa maelezo ya utaratibu kisheria kuhusu kubuniwa kwa mamlaka hiyo.

Pia anahimiza haja ya kuweka nguvu mikakati ya kurejesha mali ya umma iliyonyakuliwa kutoka kwa umma.

Mudavadi pia amepinga kubuniwa kwa serikali za kikanda (majimbo).

Miongoni mwa mapendekezo mengine pia amependekeza kufufuliwa kwa viwanda na mashirika ya kilimo yaliyoanguka, kuwekwa nguvu kwa sheria za kulinda mazingira, na kubuniwa kwa Hazina Maalum ya Kulinda Mazingira.

Kuhusu uongozi, ametaka Rais mwenye mamlaka na sharti awe kiongozi wa nchi, serikali na majeshi.

Anataka pawepo na Naibu Rais na Waziri Mkuu ambao wanateuliwa na Rais.

Amesema pakiibuka haja, Waziri Mkuu awe na naibu ama manaibu wawili.

Anataka majukumu ya Waziri Mkuu yawe wazi ili kuepuka hali ya mvutano wa kimajukumu.

Anataka Rais achaguliwe moja kwa moja na wananchi; kura moja kwa mtu mmoja.

Kuhusu ugatuzi, ametaka Kaunti 47 zibaki huku akipinga pendekezo la serikali za kikanda.

Ametaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ipewe uhuru zaidi ili kuepusha mwingiliano wa kisiasa na kwamba ifadhiliwe kutoka hazina maalum ili kuepusha mwingiliano wa kiutendakazi.