Habari Mseto

Mudavadi anyemelea Kibwana kuhusu 2022

August 31st, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU na PIUS MAUNDU

KIONGOZI wa chama cha ANC, Bw Musalia Mudavadi ameashiria kuwa huenda akaungana na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana wa Makueni kubuni muungano wa kisiasa.

Bw Mudavadi aliyezuru Kaunti ya Makueni kwa mwaliko wa Profesa Kibwana amemwambia kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuwaruhusu viongozi wengine katika eneo la Ukambani kuwania nyadhifa mbalimbali, hali ambayo wachanganuzi wanasema ni mbinu ya kumtengenezea njia gavana huyo.

Profesa Kibwana amekuwa akimpinga kisiasa Bw Musyoka, ambaye amedhibiti siasa za eneo hilo kwa muda mrefu.

Msimamo wa Profesa Kibwana ndiyo ulimfanya kuondolewa kama mwenyekiti wa Wiper na nafasi yake ikachukuliwa na aliyekuwa waziri Chirau Ali Mwakwere.

“Wakati mwanasiasa anapotangaza nia ya kutaka kuwatumikia Wakenya katika nafasi yoyote ile, hilo halipaswi kuzua uhasama,” alisema Bw Mudavadi mnamo Ijumaa, alipowahutubia wenyeji katika mji wa Wote.

Mnamo 2013 Profesa Kibwana aliwania ugavana kwa chama cha Muungano alichounganisha na Wiper kwenye uchaguzi wa 2017.

Bw Mudavadi alikuwa amealikwa na Profesa Kibwana, ambapo pia aliandamana na viongozi kadhaa wa ANC.

Gavana huyo, ambaye tayari ametangaza kwamba atawania urais mnamo 2022, alimuomba Bw Mudavadi kumlinda dhidi ya Bw Musyoka na washirika wake ambao wamekuwa wakimshambulia kutokana na tangazo hilo.

“Unapaswa kutufunza mtindo wa kisiasa unaoendelezwa katika eneo la Magharibi, ili wakati Bw Musyoka, Dkt Mutua ama mimi tunapotangaza nia ya kuwania urais, tusichukuliane kuwa mahasimu wa kisiasa,” akasema.

Washirika wa Bw Musyoka wamesema kuwa tangazo lake na Gavana Alfred Mutua wa Machakos linalenga kumharibia nafasi Bw Musyoka, ambaye pia ametangaza kuwa atawania wadhifa huo.

Kuigawanya jamii

Kulingana nao, magavana hao wawili wataigawanya jamii ya Akamba, hali ambayo itapunguza nafasi ya Bw Musyoka kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakapoondoka uongozini.

Ni kutokana na hayo ambapo Prof Kibwana alimwomba Bw Mudavadi kuwafunza viongozi wa Ukambani vile wanasiasa wa jamii ya Abaluhya huwa wanaendeleza shughuli zao za kisiasa bila kuzua uhasama.

Hata hivyo, aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama alipuuzilia mbali nia ya Profesa Kibwana na Dkt Mutua kuwania urais, akisema kuwa Bw Mudavadi anashirikiana kwa ukaribu na Bw Musyoka.

Licha ya tangazo hilo, wachanganuzi wanasema kuwa kitakuwa kibarua kigumu kwa Prof Kibwana kupata uungwaji mkono wa jamii ya Akamba, wakishikilia kuwa Bw Musyoka bado ana ushawishi mkubwa.

“Itakuwa vigumu sana kwa Prof Kibwana kumwangusha kisiasa Bw Musyoka, kwani ushawishi wake kisiasa ungalipo. Amekuwa siasani kwa muda mrefu, ikilinganishwa na Prof Kibwana, ambaye wengi bado wanamwona kama limbukeni kisiasa,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kuhusu nia ya Bw Mudavadi, wachanganuzi wanasema kuwa itabidi awatafute wanasiasa zaidi ili kuimarisha nafasi yake. Bw Mudavadi aliwania urais kwa mara ya kwanza mnamo 2013 kwa tiketi ya chama cha UDF huku akimuunga mkono Bw Raila Odinga mnamo 2017 kwa tiketi ya muungano wa NASA.