Habari

Mudavadi ashuku huenda sensa ya 2019 ikavurugwa

May 14th, 2018 2 min read

Na RUSHDIE OUDIA

SHUGHULI ya kuhesabu idadi ya watu nchini mwaka 2019 inaweza kuvurugwa iwapo mikakati madhubuti haitawekwa na kutekelezwa kuhakikisha hesabu kamili itatolewa, kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amedai.

Bw Mudavadi anataka maandalizi kamili yafanywe na kutangazwa kuhakikisha makosa yaliyoshuhudiwa kwenye sensa zilizopita hayatarudiwa.

Wakati wa sensa ya 2009, Bw Mudavadi alikuwa naibu waziri mkuu chini ya serikali ya muungano.

Anaitaka wizara ya Ugatuzi na Mipango kutangaza wazi hatua ilizochukua kuandaa sensa ya 2019 na kuhusisha washikadau wote.

Kulingana na Bw Mudavadi, sensa ya taifa inahusisha mifumo ya kisheria na kisiasa na inafaa kuendeshwa kwa njia ya kuaminika. Aliongeza kuwa kumekuwa na changamoto kuhusu shughuli hiyo inavyoendeshwa na matokeo yake.

“Matokeo ya hesabu ya watu yanaathiri moja kwa moja uchaguzi hivi kwamba yakivurugwa, inamaanisha kwamba uchaguzi utavurugwa pia. Wakenya hawatakubali shughuli iliyovurugwa,” alisema Mudavadi.

“Sensa ikivurugwa, hali hiyo itaendeleza dhuluma za kiuchumi na kisiasa. Nchi inafaa kuanza kujiandaa kwa sensa ya haki na inayoaminika,” alisema.

Kiongozi huyo wa ANC alikuwa akiongea mjini Kisumu wakati wa mkutano wa pamoja wa baraza kuu na baraza la kitaifa la ANC.

Bw Mudavadi alikumbuka kwamba 2009, aliyekuwa waziri wa mipango Bw Wycliffe Oparanya (sasa gavana wa Kakamega) alifutilia mbali matokeo ya sensa kutoka maeneo nane Kaskazini mwa Kenya (Lagdera, Mandera Central, Wajir, Mandera Mashariki, Mandera Magharibi, Turkana ya Kati, Turkana Kaskazini na Turkana Kusini) kwa sababu hayakuweza kuthibitishwa.

Ilisemekana matokeo yalionyesha watu 1 milioni zaidi ya ilivyokadiriwa na wakazi wa maeneo hayo walipoenda kortini, mahakama ilikosoa mfumo uliotumiwa.

Bw Mudavadi alisema hakutaka kuona yaliyotokea wakati huo yakirudiwa kwenye sensa ya mwaka ujao na akazitaka taasisi zinazohusika kuhakikisha hakutakuwa na udanganyifu wa sensa hiyo.

Bw Mudavadi pia anahisi kwamba kunafaa kuwa na uhusiano kati ya usajili wa watoto wanaozaliwa, usajili wa vitambulisho na paspoti, usajili wa wapigakura na usajili wa vifo.

“Kunafaa kuwa na upatikanaji wa habari za watu zinazowekwa na Shirika la Takwimu la Kitaifa ili kupata habari za kweli na tunafaa kuhakikisha sensa inatimiza viwango vya kimataifa,” alisema Bw Mudavadi.

Mipaka inafaa kuchunguzwa wakati wowote sasa baada ya miaka minane na mipya huwekwa kwa kutengemea idadi ya watu inayotambuliwa kupitia matokeo ya sensa.

“Iwapo hesabu ya idadi ya watu haitafanywa vyema, uchunguzi wa mipaka pia hautakuwa wa haki na ni chanzo cha mizozo,” alisema.