Mudavadi ataka BBI kuangaliwa upya

Mudavadi ataka BBI kuangaliwa upya

Na Gitonga Marete

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amesisitiza kuwa Bunge linapaswa kurejelea Mpango wa Maridhiano (BBI) na kutambua sehemu zisizohitaji kura ya maoni ili zitekelezwe kwa manufaa ya Wakenya.

Bw Mudavadi alitoa changamoto kwa wabunge na kuwataka kubuni sheria zitakazoangazia nyongeza ya mapato yanayotengewa kaunti ili kuhakikisha Wakenya wanapata raslimali za kutosha kwa maendeleo.

“Kuna vipengele vya BBI tunavyoweza kushughulikia bila haja ya kura ya maoni na ninawahimiza wabunge wetu kuangazia masuala haya. Kuongeza mapato kutoka kiwango cha chini cha asilimia 15 hadi asilimia 35 na kuanzishwa kwa Hazina ya Wadi kunaweza kupata msingi wake kwenye katiba kwa manufaa ya Wakenya wote,” alisema.

Kiongozi huyo wa ANC alizungumza jana alipomtembelea Gavana wa Meru, Kiraitu Murungi, kabla ya misururu ya mikutano na viongozi eneo hilo.

Aliandamana na Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala, Mbunge wa Lugari, Ayub Savula na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Kenneth Marende, miongoni mwa viongozi wengine.

Kwa upande wake, Bw Murungi alisema viongozi wa kaunti watashiriki mazungumzo na wagombea wote wa urais na kumuunga mkono yeyote atakayejali maslahi ya wakazi wa Meru.

Ziara ya Mudavadi mjini Meru imejiiri wiki mbili baada ya gavana wa kaunti hiyo kukutana na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga jijini Nairobi ambapo aliahidi kumuunga mkono.

You can share this post!

Koome aagiza kesi za miaka minne zimalizwe

Serikali kugawana malipo na wauguzi wanaotumwa UK