Habari

Mudavadi atakuwa debeni 2022 – ANC yasisitiza

September 23rd, 2020 1 min read

Na BRIAN OJAMAA

CHAMA cha Amani National Congress (ANC) kimesema kuwa kiongozi wake Musalia Mudavadi hatakuwa mwaniaji mwenza wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Badala yake, wanachana wa wa ANC kutoka maeneo ya Magharibi na Bonde la Ufa, Jumanne walisema kuwa Bw Mudavadi atawania urais.

Walisema makamu rais huyo wa zamani ana sifa zinazotakiwa kuongoza nchi hii baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu 2022.

Katibu wa chama cha ANC eneo la Magharibi, Martin Waliaula alisema kuwa Bw Mudavadi ana nafasi nzuri ya kushinda urais.

“Tumeamua kumuunga mkono kiongozi wa chama chetu na hilo halina mjadala. Wanasiasa wanaotaka kuungana naye waje na wapewe wadhifa wa mwaniaji mwenza,” akasema.

Alisema kuwa chama cha ANC kina uhakika kuwa kitaunda serikali 2022.

Bw Waliaula alimtaka Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya kuunga mkono Bw Mudavadi.

“Wamalwa yuko serikalini lakini jamii ya Waluhya haijanufaika kwa lolote. Hivyo, watu wa Magharibi wamepoteza imani naye na wanahitaji kiongozi atakayeshughulikia matakwa yao,” akasema.

Alisema kuwa Bw Mudavadi hataunga mkono kundi la ‘Tangtanga’ linalopigia debe Naibu Rais William Ruto kuwa rais wala upande wa handisheki.