Habari

Mudavadi atoa wito Serikali isaidie wachezaji wakongwe

February 19th, 2019 1 min read

Na COLLINS OMULO na JOHN ASHIHUNDU

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi ametoa wito kwa Serikali iwasaidie wanamichezo waliostaafu na hasa wanaugua.

Musalia alisema wengi wa wakongwe hao hawana uwezo wa kugharimia matibabu ya bei ghali kukabiliana na magonjwa ya uzeeni yanayowakumba.

Mwanasiasa huyo alisema Serikali kupitia kwa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) inaweza kusambaza huduma zake ili kufikia wanamichezo wa zamani waliolemewa na maradhi mbalimbali.
“Ningependa kutoa wito kwa NHIF kupitia kwa Serikali Kuu ijitolee kusaidia wanamichezo wetu waliostaafu ambao hawajiwezi kutokana na bei ghali ya matibabu nchini,” Mudavadi alisema hayo Jumatatu baada ya kumtembelea mwanasoka mkongwe Joe Kadenge ambaye alilazwa hospitalini baada ya kuugua ghafla kutokana na kifo cha mwanawe Everlyne Kadenge nchini Amerika.

Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi alipomtembelea nguli wa soka nchini Joe Kadenge katika Nairobi Hospital. Picha / Evans Habil

Naibu Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema kwamba hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza NHIF kumpa bima ya afya mkongwe huyo imemsaidia zaidi, huku akiongeza kwamba kuna wengine wengi ambao wanasumbuliwa na maradhi mbalimbali baada ya kupeperusha bendera ya taifa miaka ya awali.

“Mzee ameanza kuonyesha dalili za kupata nafuu kuliko alilivyokuwa siku za kwanza alipolazwa hapa. Tunamtakia uponaji wa haraka wakati huu tukisimama na jamii yake kwa msiba wa mawanawe aliyeaga dunia na kuzikwa nchini Amerika,” alisema.

John Anzrah ambaye ni nduguye Kadenge alisema kwamba mzee ambaye alifahamika kwa jina la ‘Kadenge na Mpira’ alipelekwa hospitalini Jumatano baada ya kupata mshtuko baada ya kifo cha Everlyne.

Bw Anzara ambaye alikuwa mwanariadha wa timu ya taifa ya mbio za kupokezana vijiti alisema Mzee Kadenge alipelekwa hospitalini na kuwekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kabla ya baadaye kupelekwa katika wodi ya kawaida ambako anaendelea kutibiwa.

“Kufikia sasa, Mzee anahudumiwa vyema na sasa yuko katika hali njema wakati huu akitarajiwa kuondoka wakati wowote. Daktari ametuambia kwamba Mzee ataruhusiwa kuondoka hospitalini wakati wowote kuanzia sasa,” alisema Anzrah.